HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 7, 2021

Watanzania waaswa kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini

 

Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wananchi pamoja na washiriki wa maonesho katika ufunguzi wa maonesho ya sita ya viwanda yaliofanyika katika viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar.WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuwapa nguvu wawekezaji wa ndani katika kuzalisha na kuinua sekta ya viwanda na Biashara.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla ameeleza hayo katika sherehe za ufunguzi wa maonesho ya sita ya bidhaa za viwanda yaliofanyika katika viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar.

Ameleza kuwa, Tanzania ina kila aina ya bidhaa zenye sifa na ubora hivyo, katika kuunga mkono jitihada za wazalishaji hakuna budi kwa watanzania kuzitumia bidhaa hizo zinazozalishwa nchini.

Aidha, Mhe. Hemed amewataka washiriki wa maonesho hayo kushiriki katika matukio mbali mbali ikiwemo mikutano ya kibiashara pamoja na kongamano la viwanda kwani kufanya hivyo kutawasaidia washiriki hao kujifunza,kubadilishana uzoefu na kukutana na wanunuzi mbali mbali wa bidhaa wanazozalisha.

Amesema serikali zote mbili (SMT na SMZ) zipo katika mchakato wa kuimarisha mazingira mazuri ya viwanda kwa lengo la kuhimili ushindani wa masoko kwa kuwa na bidhaa bora zenye viwango na zenye kuuzika ndani na nje ya nchi.

Amefafanua kwamba, katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga jumla ya shilling Billioni Themanini nan ne nukta tano (84.5) kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriliamali ili kuimarisha biashara zao.

“Na kwa vile serikali imejikita katika kuendeleza uchumi wa Buluu kati ya fedha hizo, shilling Billioni thelasini na sita nukuta tano (36.5) zitaelekezwa katika sekta ya uvuvi na mazao ya baharini hususani Mwani na Dagaa” Alisema Makamu wa Pili wa Rais

Makamu wa Pili wa Rais amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na zoezi la ukamilishaji wa ujenzi wa kiwanda cha Mwani kwa upande wa Pemba, kiwanda ambacho kwa kiasi kikubwa kitasaidia katika kuongeza thamani ya zao hilo na kuongeza pato la wananchi.

Mhe. Hemed ameleza kuwa, zao la Mwani ni moja kati ya zao kubwa la kibiashara hapa Zanzibar na limeajiri watu wengi hususani wakinamama ambao wanafanya kazi nzuri.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban amesema tokea kuasisiwa kwa maonesho hayo mwaka 2016 jumla ya wenye viwanda 500 wameshiriki kwa kuunga mkono maonesho hayo, ambapo kwa mwaka huu Washihiri 113 wameweza kushiriki, ikiwemo viwanda 10 vya Zanzibar na viwanda 23 kutoka Tanzania bara.

Amesema lengo la kuwepo wa maonesho hayo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda nchini, ambapo wananchi kupitia maonesho hayo hushajiika kujionea na kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, na kuamsha ari kwa wananchi kuanzisha viwanda mbali mbali nchini kwa lengo la kuinua sekta hiyo.

Akitoa salamu kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Serikali ya Jamuhuri ya Muungani wa Tanzania Bw. Alfred Mapunda amesema kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wenye viwanda kuweza kutangaza biashara zao, na kuweza kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza uchumi kupitia uchumi wa viwanda, na kuwataka wazanzibari kutumia fursa hiyo, kuutangaza uchumi wa buluu unaotokana na viwanda nchini.

Katika uzinduzi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukagua mabanda mbali mbali ya maonesho ili kujionea namna wananchi walivyoshajiika katika kukuza sekta ya viwanda nchini.

Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema “Tumia bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania”

 Hemed akikata utepe kuashiria kuyazindua rasmi maonesho ya sita ya Viwanda ikiwa ni shamrashamra ya sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Alfred Mapunda akizungumza katika maonesho ya sita ya Viwanda yaliofanyika katika Viwanja vya Maisara ambapo Katibu Mapunda alimuawakisha Mhe. Waziri Prof. Kitila Mkumbo.
Waziri wa Biashara na maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban akizungumza na wananchi na washiriki waliohudhuria katika maonesho ya sita ya Viwanda yaliofanyika katika Viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad