MADAKTARI WALIOPATIWA MAFUNZO NA WCF WAONGEZEKA NA KUFIKIA 1,323 NCHI NZIMA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 4, 2021

MADAKTARI WALIOPATIWA MAFUNZO NA WCF WAONGEZEKA NA KUFIKIA 1,323 NCHI NZIMA

 NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mbeya.

IDADI ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi imepanda na kufikia 1,323 nchi nzima, Mkurugenzi Mkuu wa, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema.

Dkt. Mduma ameyasema hayo  wakati wa mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na WCF ili kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya jinsi ya kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kutoka mikoa saba ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa.

“Tukiwa tunaelekea mwaka wa saba tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu yake, ninyi ambao mmepatiwa mafunzo hapa, mnafanya idadi ya madaktari wenye ujuzi wa kufanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,323 kwenye mikoa yote Tanzania Bara.” Alisema.

Aidha Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema madaktari hao walijifunza mambo mbali mbali ikiwemo sheria ya fidia, jinsi ya kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao, kusajili waajiri na namna wanavyoweza kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa njia ya mtandao, namna ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi na Mafao yatolewayo na Mfuko,

Kwa upande wao, washiriki hao waliupongeza Mfuko kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wameeleza yamekuwa na manufaa makubwa kwao.

 “Nimejifunza mambo mengi ambayo nilikuwa siyafahamu,mfano sasa nimejua ya kwamba mtu anapokuwa amepata ajali itakayompelekea kupata ulemavu atastahili kufanyiwa tathmini pale tu atakapofikia kiwango cha juu cha kupona yaani maximum medical improvement.”. Dkt. Adolph Daudi Ntilagana, Hosptali ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi alisema.

Mshiriki mwingine Dkt.Pronent Mtei kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya alisema mafunzo hayo yamembadilisha kwani hivi sasa ameelewa kwamba Mfuko unaweza kumpatia matibabu au fidia mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.

“Nimejifunza na kuelewa tofauti ya magonjwa yatokanayo na kazi na yale ambayo hayatokani na kazi, hivyo itakuwa rahisi kwangu mteja anapokuja kwa changamoto ya maradhi kuweza kumtambua kama tatizo lake lina vigezo au la kwa mujibu wa mwongozo wa WCF.” Alisema Dkt. Mtei

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, (MZRH) Dkt. Godlove Mbwanji ambaye ndiye aliyafunga mafunzo hayo aliwaasa madaktari na watoa huduma za afya kuzingatia yale waliyojifunza wakati watakaporejea kwenye vituo vyao vya kazi.

“Mafunzo haya yatatusaidia sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini kuweza kufanya tathmini sahihi ambayo itauwezesha Mfuko kutoa fidia stahiki na  kwa wakati.” Alisisitiza.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akifuatilia majadiliano ya vikundi mwisho mwa mafunzo hayo.
Majadiliano ya vikundi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dkt.Godlove Mbwanji (wapili kushoto) akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo hayo, Dkt. Marther Chacha huku Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Juma Mabrouk (kushoto) akishuhudia.
Baadhi ya washiriki.
Dkt. Adolph Daudi kutoka Hospitali ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake.
 Dkt. Francis Chila (kulia) na Innocensia William wote kutoka WCF wakipitia dodoso maalum tayari kuwagawia washiriki kwa uelewa wa mafunzo
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar akijibu maswali ya washiriki.
Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, (MZRH) Dkt. Godlove Mbwanji akizungumza na washiriki.
Afisa Tathmini za madai, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Matilda Rusibamayila (wakwanza kulia waliosimama) akifuatilia majadiliano ya vikundi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad