CHUO CHA ARDHI TABORA CHATAKIWA KUTANGAZA KAZI ZAKE ZA UCHAPISHAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 6, 2021

CHUO CHA ARDHI TABORA CHATAKIWA KUTANGAZA KAZI ZAKE ZA UCHAPISHAJI


 

Na Munir Shemweta, WANMM TABORA

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekitaka Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kuitangaza idara yake ya uchapishaji ili iweze kufahamika na kutumika kwa shughuli za uchapishaji yakiwemo machapisho ya serikali.

 

Dkt Mabula alisema hayo tarehe 5 Novemba 2021 alipofanya ziara katika chuo cha ARITA kukagua utendaji kazi  akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tabora.

 

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo, Chuo cha Ardhi Tabora kinatakiwa kijitangaza hasa idara yake ya uchapishaji kwa kuwa kazi za idara hiyo zinaweza kukiingizia mapato chuo itakayoweza kutumika katika shughuli mbalimbali za  maendeleo ya chuo.

 

 "Tungetumia sehemu ya printing ya chuo hiki tungweza kupata fedha nyingi hivyo tunatakiwa tuitangaze idara hii ya uchapishaji kwa kuwa Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali haiwezi kufanya kazi zote na pale ofisi hiyo itakapozidiwa basi chuo hicho kifanye kazi hiyo". Alisema Dkt Mabula

 

Mkuu wa idara ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji wa Chuo cha Ardhi Tabora Praygod Lema alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa, idara hiyo pamoja na kufanya kazi kubwa ya uchapishaji baadhi ya nyaraka za Wizara ya Ardhi na zile za halmadhauri ya jiji la Dodoma bado ina changamoto ya mashine ya uchapishaji kutokana na zilizopo sasa kutoendana na kasi ya mahitaji ambapo aliomba idara hiyo kupatiwa mashine nyingine ya kisasa.

.

"Pamoja na changamoto mlizokuwa nazo kuna haja ya kufanya matangazo na mnaweza kutumia hata vyombo vya habari ili muweze kupata kazi na kuingiza fedha maana bila ya hivyo mtaendelea kuwa na changamoto za kifedha " alisema Dkt Mabula.

 

Hata hivyo, Dkt Mabula alikipongeza Chuo cha ARITA kwa kazi nzuri pamoja na changamoto inazozikabili katika utendaji kazi wake na kuutaka uongozi wa chuo kufuatilia maombi mbalimbali inayoyapeleka Wizarani kwa ajili ya kusaidiwa.

 

Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Donald Rweramila alisema, pamoja na  chuo cha ARITA kufanya kazi ya uchapishaji lakini hakina Maabara ya Fani ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji kwa ajili ya mafunzo ya vitendo jambo alilolieleza kuwa linawafanya wanafunzi kutumika zaidi uandani.

 

Akigeukia zoezi la urasimishaji makazi holela ambapo Chuo hicho kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo Donald Rweramila kimepatiwa  Milioni 644.5, Dkt Mabula alikitaka chuo cha ARITA kushirikisha wadau kabla ya kuanza kazi hiyo kwa kufanya mikutano ili  kujenga ufahamu na kubainisha kuwa, mazoezi mengi ya urasimishaji makazi holela yanakwama kutokana na kutoshirikisha wadau.

 

"Nitarajia mtafanya mikutano na wadau na mazoezi mengi ya urasikishaji makazi holela yanakwama kutokana na kutoshirikisha wananchi na usiposhirikisha na kujua changamoto hamuwezi kufanikiwa". alisema Dkt Mabula

 

Chuo cha Ardhi Tabora kinatarajia kufanya mazoezi ya urasimishaji makazi holela katika maeneo ya Tabora, Geita na Kasulu mjini mkoani Kigoma na tayari chuo hicho kimeshatambua viwanja 27,000. 

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia baadhi ya machapisho yaliyofanywa na Chuo cha Ardhi Tabora kupitia idara yake ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji Chuo cha Ardhi Tabora alipofanya ziara katika chuo hicho jana. Nyuma yake ni Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Donald Rweramila
Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Sanaa, Ubunifu na Uchapishaji Chuo cha Ardhi Tabora Playgod Lema (Kushoto) alipofanya ziara katika chuo hicho jana.
Wajumbe wa menijementi ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake katika chuo hicho.
Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na uongozi wa Chuo cha Ardhi Tabora wakati wa ziara yake mkoani Tabora jana. Kushoto ni Mkuu wa Chuo Donald Rweramila
Naibu Waziri waArdhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) Donald Rweramila kuelekea kukagua mashine za uchapishaji za chuo hicho wakati wa ziara yake chuoni hapo jana

 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad