HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 21, 2021

Benki ya CRDB yaing’arisha Tanzania katika tuzo za sekta ya fedha za Afrika Mashariki

 
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Viwango vya Mahesabu ya Umma ya Kenya (PSASB), Stephen Masha (kushoto) akimkabidhi tuzo ya uwasilishaji bora wa taarifa za fedha kwa mwaka 2019/2020 katika sekta ya benki kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Meneja wa Idara ya Fedha ya Benki ya CRDB, Aldo Kamugisha.
 
========    ========     =======

Benki ya CRDB kwa mara nyingine tena imeibuka mshindi wa jumla wa uwasilishaji bora wa taarifa za fedha kwa mwaka 2019/20 katika sekta ya benki kwa ukanda wa Afrika Mashariki na nyingine ni tuzo ya uwasilishaji bora wa taarifa za fedha kwa upande wa Tanzania. Ushindi huo umepatikana katika Tuzo za FiRe (Financial Reporting) zilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Nairobi nchini Kenya

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo ikiwa ni siku chache baada ya kupokea tuzo nyingine zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kama taasisi ya fedha iliyoongoza kwa kuwasilisha Taarifa ya Fedha bora kwa mwaka 2019/2020 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema tuzo hizo ni muendelezo wa uthibitisho wa umahiri wa Benki katika uwasilishaji wa taarifa za fedha zinazozingatia viwango vya kimataifa.
“Tumefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali hii ni pamoja na kuboresha mifumo yetu ya kukusanya na kuandaa taarifa. Tumeweza pia kuunganisha mfumo wetu wa utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za fedha (IFRS), hii pia imechangia Benki yetu kuwa bora zaidi,” alisema Nshekanabo.
 
Nshekanabo alibainisha kuwa ushindi huo pia unatokana na Benki ya CRDB kuwa na wafanyakazi wenye weledi na  mfumo bora wa uongozi  unaozingatia weledi, uwazi na ukweli katika uandaaji wa taarifa za kifedha huku suala la uwajibikaji na kiwango cha juu cha uadilifu wa takwimu kikiwa ni moja kati ya vipaumbele vikuu katika maandalizi ya taarifa za fedha.  

Tuzo za FiRe (Financial Reporting) ni moja kati ya tuzo zenye hadhi na kushindaniwa na makampuni mengi makubwa katika masuala ya uwasilishaji wa taaifa za fedha. Tuzo hizi hutolewa kila mwaka zikishirikisha Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Kenya (CMA),  Taasisi wa Wahasibu wa Kenya (ICPAK), Soko la Mitaji la Nairobi (NSE), Bodi ya Usimamizi wa Viwango vya Mahesabu ya Umma ya Kenya (PSASB) na Mamlaka ya Stahili za Wastaafu ya Kenya (RBA).
Kwa zaidi ya miaka 18 iliyopita, tuzo za FiRe zimetambua na kuwatunukia makampuni ambayo yamefanya vizuri katika uwasilishaji wa taarifa za fedha katika ukanda wa Afrika Mashariki. Tuzo hizi zimekua zikihamasisha makampuni kuwekeza katika kuwa bora na kujifunza taratibu bora za uwasilishaji wa taarifa za fedha.  Tuzo hizi pia zimekua zikilenga kuhamasisha uwajibikaji, uwazi na ukweli katika taasisi za serikali, binafsi pamoja na taasisi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad