Na John Walter-Monduli.
Serikali
mkoani Arusha imechukua Sampuli 17 ya Ng'ombe waliokufa Kiutata katika
kijiji cha Popo Migungani A eneo la Mto wa Mbu wilaya ya Monduli ili
kujua chanzo cha vifo hivyo.
Daktari
wa Mifugo mkoa wa Arusha Dr. Sabas Shange amethibitisha kufa kwa
ngo'mbe hao 17 na kufanya uchunguzi wa awali kuona chanzo ni nini ambapo
ameeleza kuwa wamefanya uchunguzi wa mazingira kwa kuangalia historia
ya mifugo ilipoanzia mpaka tatizo lilipotokea na kuzichukua baadhi ya
sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa Kina. "Lakini tumejaribu kumpasua
mmojawapo kujiridhisha" alisema Dr. Shange
Kufuatia
hilo, Wafugaji katika maeneo hayo wamemuomba mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan na mwenyekiti wa wafugaji Taifa wapokee kilio chao na
kuangalia kwa jicho la pili kwa kuwa wamepata hasara kubwa.
Mmoja
kati ya wafugaji ambao mifugo yao imekufa ni Baraka Komite anasema
ndani ya dakika kumi akiwa anachunga aliona Ng'ombe wa kwanza anaruka
kisha kuanguka wakadhani kuwa ameumwa na Nyoka.
"Tulimkimbilia
tukamkamata tuangalie nini kimetokea,lakini wakati tunamuangalia huyu,
mwingine akaruka mara ghafla wakaanza kuanguka wengi"alisema Komite
Mfugaji
huyo ameendelea kusema kuwa huenda ni binadamu wanaangamiza mifugo yao
kwa sumu na kwamba hawatalivumilia jambo hilo huku akimuomba Rais Samia
Suluhu Hassan kuwaangalia wafugaji kwani hiyo ni mara ya tatu kutokea
kwa tukio kama hilo.
"Wiki
mbili zilizopita kuna ng'ombe alikufa kwa ajili ya sumu na haijulikani
nani amempa, hata sisi wafugaji pia ni wataalamu wa kujua mimea inayoua
mifugo, kwa hiyo mnapotuambia kwamba kuna mimea imeua ng'ombe ni kitu
ambayo haiwezi kuingia akilini maana ile mimea inaota kipindi cha
Masika" alisisitiza Komite
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Popo John Sulle amesema muda wa saa saba na nusu mchana
alipata taarifa kutoka kwa wananchi na alipofika alikuta ng'ombe saba
wamelala chini wakaanza kuwapa maziwa na maji huku katika eneo hilo pua
zikinusa harufu nzito kama ya sumu ambapo alitoa taarifa polisi na kwa
viongozi wengine wa kijiji.
Naye
mwenyekiti wa Kijiji cha Losirwa Yamati Laizer ameiomba serikali
kufanya uchunguzi wa kina kwenye sampuli walizozichukua ili kujua sababu
ni nini.Diwani wa kata ya Esilalei Mheshimiwa Lemia ameliomba jeshi la
Polisi kufanya upelelezi wa kina juu ya tukio hilo.
Mkuu
wa wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe ambaye alifika katika eneo hilo
kuwafariji wahanga aliwapa pole na kuwataka kuendelea kuwa watulivu
wakati wataalamu wanashughulikia vipimo katika maabara ili kubaini nini
kilichoua mifugo hiyo.
No comments:
Post a Comment