Serikali Yaeleza fursa zitokanazo na bwawa la Mwalimu Julius Nyerere - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 5, 2021

Serikali Yaeleza fursa zitokanazo na bwawa la Mwalimu Julius Nyerere

 


Mkurugenzi wizara ya Nishati Oscar Kashaigili  akieleza faida za bwawa la Mwalimu Nyerere kwa wadau wanaojadili faida za mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere nchini.
Mkufunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe na Mwananuchumi, Profesa Honest Ngowi akizungumza wakati wa kujadiliana faida za mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere nchini.

Na Mwandishi Wetu
BWAWA la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), linatoa faida sasa kwa wananchi na litaendelea kutoa faida baada ya ujenzi kukamilika Juni mwaka 2022, mbali na kuzalisha umeme wa megawati 2115, imeelezwa.

Akiwasilisha mada kwenye kongamano la kuangalia faida za bwawa hilo mbali ya kuzalisha umeme baada ya kukamilika, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mziumbe, Tawi la Dar es Salaam, Profesa Honest Ngowi amesema leo jijini Dar es Salaam kwamba kwa kuangalia mabwawa matatu duniani likiwemo la Rusumo, kuna faida lukuki kwa wananchi tangu mradi unaanza na hata baada ya kumalizika.

Amesema Bwawa la Nyerere kama yalivyo mabwawa mengine duniani litasaidia kudhibiti mafuriko, kuendesha shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kutoa maji kwa ajili ya viwanda na shughuli za majumbani.

Amesema kama ambavyo hadi sasa bwawa hilo limetoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 7,000, hata baada ya kukamilika ajira zitaendelea ingawa zile zisizo za moja kwa moja zitapungua.

“Kutakuwa na shughuli nyingi hata baada ya mradi kukamilika kama uvuvi, utalii na kadhalika na hivyo Watanzania, hususani walio karibu na eneo la bwawa, wataendelea kunufaika na uwepo wa bwawa hilo,” amesema.

Amesema faida nyingine za bwawa hilo ambazo zimeendelea kuwepo tangu mradi ulipoanza ni kujenga miundombinu kama barabara, hospitali na huduma za umeme.

“Hata kama barabara zilijengwa kwa ajili ya mradi, baada ya mradi kukamilika zitaendelea kunufaisha wananchi,” amesema Profesa Ngowi

Naye Oscar Kashaigiri aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, amesema katika mada yake kwamba Bwawa la Nyerere linasababisha uwepo wa ziwa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 914 na hivyo linaweza kuwa ni ziwa la nne au la tano kwa ukubwa nchini.

Amesema ziwa hilo pekee litavutia shughuli nyingi za kiuchumi kama yalivyo maziwa mengine kama utalii, uvuvi wa kawaida na wa uvuvi wa kitalii na sekta ya bishara kwa ajili ya watu watakaondesha shughuli mbali za kiucumi katika eneo hilo.

“Shughuli za uvuvi zitafanyika kwa sababu litakuwa ziwa kubwa na pengine serikali itapandikiza samaki zaidi kwenye ziwa hilo,” amesema.

Amesema mbali na umwagiliaji, maji yakishatumika kuzalisha yataendelea kutumika kwa ajili ya viwanda na matumizi mengine ya kiuchumi na majumbani.

Kongamano la siku mbili linalojadili manufaa ya JNHPP baada ya mradi huo kukamilika pamoja na namna Tanzania itakavyoongeza mafuta ya kupikia ili kukabili mahitaji limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

Kongamano linashirikisha maofisa wa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na kilimo, ufugaji, uzalishaji wa mafuta ya kupikia na kadhalika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad