Benki ya CRDB yapata Faida ya Shilingi 238 Bilioni - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 31, 2021

Benki ya CRDB yapata Faida ya Shilingi 238 Bilioni

Benki ya CRDB imetangaza ukuaji mkubwa katika matokeo yake ya fedha ya robo ya tatu ya mwaka iliyoishia Septemba 30, 2021. Katika kipindi hicho Benki hiyo imeshuhudia ukuaji katika viashiria vyote vya utendaji wa kifedha, na kuendeleza matokeo mazuri ambayo iliyapata katika robo mbili za kwanza katika mwaka huu wa fedha.

Katika ripoti hiyo iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 29 2021, Benki ya CRDB iliripoti ongezeko la 39.9% ya Faida Kabla ya Kodi kufikia Sh. 238 bilioni ikilinganishwa na Sh. 170 bilioni iliyorekodiwa mwishoni mwa robo ya tatu ya 2020. Faida Baada ya Kodi iliongezeka kwa asilimia 39.2 hadi Sh. 168 bilioni, kutoka TZS 120 bilioni iliyorekodiwa mwaka uliopita, hivyo kupelekea mapato yatokanayo na uwekezaji wa wanahisa kukua kwa 29.3% ikilinganishwa na 20.9% iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mizania ya Benki hiyo iliendelea kuimarika, ambapo ilifikisha jumla ya rasilimali za Sh. 8.1 trilioni, ikiwa ni ongezeko la 20.1% zaidi ya Sh. 6.8 trilioni iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Ikiendelea kushuhudia matokeo chanya ya mkakati wake wa uboreshaji biashara kidijitali, ambapo mtandao wa CRDB Wakala uliongezeka kwa zaidi ya 18.5%, Amana za Wateja ziliongezeka hadi Sh 6.0 trilioni, ikiwa ni ongezeko la 20.2% kutoka Sh. 5.0 trilioni mwaka jana.

Mkakati wa Benki ya CRDB katika udhibiti wa hatari, na ufanisi wa mkakati wake wa kidijitali wenye kuzingatia mahitaji halisi ya wateja, ulisaidia kuleta chachu ya ukuaji wa mikopo na kuweza kudhibiti gharama za uendeshaji katika kipindi hicho. Uwezeshaji kupitia mikopo kwa wateja binafsi na biashara uliimarika katika robo ya tatu ya mwaka. Jumla ya mikopo iliyotolewa ilifikia Sh. 4.6 trilioni, takribani ongezeko la 22% kutoka robo ya mwaka iliyopita. Ubora wa mikopo katika robo hiyo pia ulibaki kuwa mzuri, ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulishuka kufikia 3.5% kutoka 4.6% iliyorekodiwa mwaka jana. 

Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema, "Kwa mara nyingine tena, Benki imeonyesha uthabiti katika kutekeleza ahadi yake kwa wanahisa, wateja, na jamii, ikidhihirishwa na matokeo mazuri iliyopata katika robo ya tatu ya mwaka. Tunalenga katika kuendeleza ufanisi huku tukidumisha udhibiti thabiti, na tuna uhakika wa kufikia malengo tuliyojiwekea katika mkakati wetu wa biashara kwa mwaka 2021."

"Mapato halisi ya riba yaliongezeka kwa 11.1% hadi Sh. 570 bilioni katika kipindi cha miezi tisa, hivyo kuakisi uboreshaji wa uchumi wa nchi wakati serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kukabiliana na COVID-19. Vile vile, mapato yetu yasiyo ya riba yaliongezeka kwa 12.1% kufikia Sh. 229 bilioni, yakichangiwa zaidi na mkazo tuliouweka katika huduma za kidijitali," Nsekela alifafanua. 

Akielezea zaidi juu ya utendaji wa Benki ya CRDB, Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Fredrick Nshekanabo, alisema, "Uwekezaji wa Wanahisa uliongezeka kwa 14.7% kufikia Sh. 1.1 trilioni kutoka Sh. 974 bilioni mwaka 2020, hivyo kuifanya benki kuwa na uwezo mkubwa kimtaji. Uwiano wa Mapato na Gharama uliimarika hadi 55.6%, wakati uwiano wa mapato na mali uliimarika zaidi kwa 5.5%, ikionyesha utendaji thabiti wa kifedha katika robo ya tatu ya mwaka.”

Akizungumzia matarajio ya kipindi cha mwaka kilichosalia, Nsekela alisema, "Kwa kuangalia mbele, tuko tayari kwa ukuaji mkubwa wa mapato kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2021, ukuaji unaochochewa na huduma zetu za kifedha za kidijitali, mizania thabiti na ufanisi wa kiutendaji. Tutaendelea kutumia vizuri uimara wetu wa mizania na msingi wa wateja mbalimbali ili kutoa utendaji mzuri na kuongeza thamani kwa wanahisa wetu."

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad