HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 10, 2021

WAZIRI BASHUNGWA AIGIZA COSOTA KUANDAA MPANGO MKAKATI WA MAKUSANYO YA MIRABAHA


Na Anitha Jonas -  COSOTA, Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa ameigiza Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuandaa mpango mkakati wa makusanyo ya mirabaha pamoja na takwimu za maeneo yanayotakiwa kulipa mirabaha na kuziwasilisha wizarani mwisho mwa mwezi Septemba.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Septemba 10, 2021 Jijini Dodoma katika kikao chake na Kikosi kazi cha kukusanya maoni ya wadau katika Kanuni ya Leseni na Maonesho kwa Umma ya 2021 kutoka COSOTA kikiwasilisha taarifa ya maoni ya wadau kwa kanuni hiyo.

"Katika kikao ambacho tutakutana baada ya wiki mbili hizi mje na mkakati huo lazima tujue tunakusanya kwa akina nani na wako wapi pamoja na idadi yao, pia ongezeni kasi ya ukusanyaji wa mirabaha Disemba tunatakiwa kutoa gawio kubwa,"alisema Mhe.  Bashungwa.

Amesisitiza kuwa anahitaji kupata makadirio ya makusanyo ya mirabaha hiyo kwa mwaka huu wa fedha  na  kuanzisha utaratibu ambao atakuwa akifuatilia hali ya makusanyo hayo kwa kila mwezi kwa kuhakikisha anapata taarifa.

Pamoja na hayo naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul aliitaka COSOTA kuhakikisha inajipanga zaidi na kujenga utaratibu wa kushirikiana na mashirikisho na vyama vinavyosimamia maeneo ya kukusanya mirabaha ili kutengeneza mazingira rafiki ya zoezi hili la ukusanyaji.

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Hassan Abbasi alifafanua kuhusu suala la kukamilika kwa mfumo utakao kuwa ukihesabu na kutambua nyimbo zinazochezwa katika vituo vya Redio kuwa unatarajia kukamilika mwezi Oktoba na ndiyo utaanza kufanya kazi rasmi.

" COSOTA mna kazi kubwa ya kufanya na kuhakikisha mnakusanya fedha za kutosha ili gawio la mwezi Disemba liwe lenye hamasa kwa Wasanii wetu ni imani yangu kuwa kwa Kanuni hii mpya na viwango hivi mlivyopanga kuwa vinalipika kikubwa katika hili ni kuweka mifumo ya kiteknolojia ambayo itarahisisha makusanyo hayo,"alisema Dkt.Abbasi.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa akitoa agizo kwa Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuandaa mpango mkakati wa makusanyo ya mirabaha kwa mwaka 2021/2022 na takwimu za maeneo yanayotakiwa kulipa mirabaha leo Septemba 10, 2021  katika kikao chake na kikosi kazi cha Kilichokuwa kikikusanya maoni ya Kanuni  ya Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa Umma 2021 kutoka COSOTA (hawapo pichani) leo Septemba 10,2021 Jijini Dodoma
Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul akisisitiza COSOTA kuongeza nguvu kazi katika makusanyo ya mirabaha kuelekea gawio la mwezi Disemba , katika kikao cha kikosi kazi cha COSOTA  kilichokuwa kinakusanya maoni ya Kanuni ya Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa Umma 2021  kilichofanyika leo Septemba 10, 2021  Jijini Dodoma.

Mwanasheria kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA ) Lupakisyo Mwambinga wa pili kushoto akiwasilisha maoni ya wadau katika mapendekezo ya Kanuni ya Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa Umma 2021 kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa leo Septemba 10, 2021 Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad