HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 17, 2021

Mjamzito mwenye selimundu abadilishiwa chembe nyekundu za damu

 

Kwa mara ya kwanza, wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamebadilisha chembe nyekundu za damu kwa mama mjamzito mwenye ugonjwa wa selimundu kwa kutumia mashine za kisasa (Spectra Otia).

Wataalamu wataendelea kumbadilishia damu nyekundu Bi. Easter Gabriel hadi atakapojifungua lengo ni kuhakikisha anaendelea kuwa na afya bora na kujifungua salama.

“Nimekuwa na tatizo hili tangu nilipozaliwa na hivi sasa nina ujauzito wiki 28, lakini nikawa napata maumivu ambayo hayaishi hata nichomwe dawa ya aina gani. Nashukuru wataalamu wa afya Muhimbili, wamenishika mkono, hawakuwahi kuniangusha, walikuwa wananiambia mimi sazai, lakini hawa wataalamu wamenisaidia, pia naishukuru Serikali,” amesema Bi. Easter.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Mbonea Yonazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amesema kabla ya kupatiwa mashine hizo, walikuwa wakimbadilisha mgonjwa chembe nyekundu za damu kwa kutumia njia ya kawaida ambayo ilikuwa ikichukua saa sita wakati hivi sasa kwa kutumia teknolijia mpya ni saa mbili tu na nusu.

Dkt. Yonazi amesema mama huyo amebadilishiwa chembe nyekundu za damu kutokana na chembe hizo kuwa na kasoro ambazo huaribu mimba changa, kujifungua kabla ya wakati na kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu.

Amesema kutokana na hali hiyo, chembe nyekundu za damu zenye kasoro pia zinasababisha maumivu makali ya mara kwa mara katika sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha mgonjwa kushindwa kuudhuria kazi, masomo na shughuli nyingine mbalimbali kutokana na kulazimika kulazwa.

Amefafanua kwamba kasoro ya vinasaba anavyorithi mgonjwa husababisha kutengenezwa kwa haemoglobini iliyojikunja na kusababisha chembe nyekundu (kibebeo) kujikunja.

“Hali hii husababisha chembe nyekundu za damu zijikunje na kuwa na umbile l a mwezi mchanga na chembe nyekundu zilizojikunja haziwezi kupita kwenye mishipa ya damu, hukwama na kusababisha wagonjwa kubadilishiwa damu na kuwekewa damu isiyokuwa na selimundu ili kuondoa athari  mbalimbali za selimundu,” amesema Dkt. Yonazi.

 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Mbonea Yonazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanikiwa kubadilisha chembe nyekundu za damu kwa mama mjamzito mwenye ugonjwa wa selimundu na afya yake kuendelea vizuri. 
Bi. Easter Gabriel (25) akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako amebadilishiwa   chembe nyekundu za damu.
Bingwa wa Magonjwa ya Damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Matilda Ngarina akizungumza kuhusu afya ya mama mjamzito aliyepatiwa matibabu kutokana na kuwa na tatizo la selimundu. Kushoto ni Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Neema Lubuva na Dkt. Yonazi, wote wa Hospitali ya Muhimbili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad