MIPANGO SERA MAKINI CHACHU YA MAENDELEO - RAIS MWINYI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 23, 2021

MIPANGO SERA MAKINI CHACHU YA MAENDELEO - RAIS MWINYI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Taifa haliwezi kusonga mbele bila ya kuwepo mipango na sera makini katika sekta ya elimu inayolenga kuiwezesha na kuiongoza jamii kuelekea maendeleo ya kweli.

Rais ameyasema hayo leo katika hotuba yake iliyowasilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, katika kilele cha maadhimisho ya 57 ya Sherehe ya Elimu Bila Malipo, zilizofanyika ndani ya Kiwanja cha Gombani, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema Mapinduzi ya Januari 1964, chini ya Jemedari Hayati Mzee Abeid Amani Karume, yalilenga kumjengea uwezo Mzanzibari na kumkomboa kila mwananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kiuchumi na kimaendeleo kupitia uwekezaji katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya 8 ni kuendeleza matunda ya mapinduzi ambayo ni pamoja na kumpatia kila mtoto wa visiwa hivi elimu bure, kumuendeleza kielimu na kumuwezesha katika kukabiliana na ushindani wa soko la ajira ulimwenguni, Zanzibar ikiwa sehemu ya dunia inayohitaji kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko.

Katika utekelezaji wa azma hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikishirikiana na wadau mbali mbali wa elimu ili kuleta tija  na mabadiliko katika sekta ya elimu nchini.

Mheshimiwa Dkt Mwinyi ameeleza ongezeko kubwa la mahitaji ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye sifa ambapo jumla ya Tsh 11,105, 850, 239/= zimetumika kwa mwaka 2019/2020 , kuwapatia mikopo wanafunzi 4,040 wakiwemo wapya na wanaoendelea na masomo.  

Akibainisha mikakati ya kuimarisha sekta ya elimu Mhe. Dkt Mwinyi amesema Serikali imeamua kuifanyia mapitio Sera ya Elimu ya mwaka 2006, na kuifanyia marekebisho ya mwaka 2020, kwa kuzingatia mipango mbali mbali ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo Malengo ya Dunia ya Maendeleo Endelevu, Uchumi wa Buluu, Michango ya Wazee katika Elimu, na Dira ya 2050 ya Zanzibar.
 
Aidha Mheshimiwa Rais Dokta Mwinyi ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar juu ya juhudi mbali mbali inazozichukua pamoja na kuwapatia vijana taaluma katika fani mbali mbali zikiwemo za udaktari, ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuhamasisha maendeleo.

Akiongelea juu ya haja ya kukabiliana na tatizo la ajira na uhaba wa walimu hapa visiwani, Mheshimiwa Dkt Mwinyi amesema, “Serikali inatambua kuwa kuimarika kwa miundombinu pekee haitoshi katika kuleta maendeleo ya sekta ya elimu ila uimarishaji huo unatakiwa kwenda sambamba na uimarishaji wa raslimali watu”.

Akiainisha baadhi ya maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 57 ya Elimu bila Malipo, Mhe Dokta Mwinyi amesema, “kabla ya mapinduzi Zanzibar ilikuwepo na skuli (1) ya maandalizi yenye wanafunzi 60, skuli 62 za msingi zilizokuwa na wanafunzi 24,334 na skuli 5 za sekondari zilizokuwa na wanafunzi 1,038, leo hii taasisi za elimu zimeenea kwa wingi, sasa hivi tuna jumla ya skuli 312 zinazotoa elimu ya maandalizi zenye wanafunzi 40,479, takwimu pia zinaonyesha skuli zinazotoa elimu ya msingi ni 333 zikiwa na jumla ya wanafunzi 362,657, ama kwa upande wa sekondari tuna jumla ya skuli 218 zenye jumla ya 116,227, na tuna vyuo vya ualimu viwili vyenye wanafunzi 1,221”.

Ametaja pia maendeleo hayo kuwa ni pamoja na uwepo wa vyuo vikuu vinne ambapo kimoja ni cha Serikali, sambamba na ongezeko la ufaulu wa Sekondari na elimu ya Juu kutoka asilimia 33.92 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 40.5 kwa mwaka 2021 tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964.  

Katika kukabiliana na janga la CORONA na maradhi ya UVIKO-19, Rais Dkt Hussein Mwinyi ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuzingatia maagizo yote yanayotolewa na wataalamu ili kujikinga na balaa hilo linaloendelea kuiathiri dunia.

Pia ameweka msisitizo maalumu katika kuzingatia hadhi na heshima ya mwalimu katika jamii, akisema bila ya kuyapa umuhimu hayo, si rahisi kuifikia dhamira ya mendeleo ya kweli kupitia sekta ya elimu.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohamed Said, amesema wizara yake ipo katika mageuzi makubwa kuhakikisha sekta hiyo inaimarika kwa mujibu wa mahitaji na kutoa fursa muhimu ya maendeleo ili kuendana na kasi ya mabadiliko duniani.

Amepongeza juhudi na utayari wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kushiriki na kuchangia elimu, hali ambayo inahamasisha na kujenga matumaini katika uendeshaji wa sekta hiyo muhimu ya maendeleo.

Kabla ya hapo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor akiwasilisha salamu za wananchi wa mkoa huo ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutokana na juhudi za kuhamasisha maendeleo ya elimu nchini kama ilivyokuwa dhamira ya waasisi wa Mapinduzi.

Maadhimisho hayo yaliyoanza tangu tarehe 2 Septemba 2021 yalijumuisha harakati na shamrashamra mbali mbali zikiwemo za Sanaa, utamaduni, makongamano ya kitaaluma, mashindano ya michezo, maonyesho ya ufundi na kazi za amali, yaliyowajumuisha wadau wa sekta ya Elimu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Viongozi mbali mbali wamejumuika katika hafla hiyo ambao ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Dokta Saada Mkuya Salum, na Waziri wa Kilimo na Mifugo Mhe. Dokta Sudi Nahoda.  

Siku ya Elimu Bila Malipo huadhimishwa kitaifa kila ifikapo tarehe 23 Septemba, kufuatia tamko la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, la Elimu Bila Malipo, lililotaka Watoto wote wa visiwa vya Unguja na Pemba wasome bila kulipia.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad