Na John Mapepele, WHUSM
Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni msimamizi na mratibu
wa shughuli zote zinazohusu maendeleo ya utamaduni nchini, leo Agosti
18, 2021 imefanya kikao na wadau mbalimbali nchini ili kutoa maoni ya
Mwongozo wa Maadili ya Taifa na Utamaduni wa Mtanzania katika ukumbi wa
Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho,
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Emmanuel Temu,
ametanabaisha kuwa lengo la kikao hicho ni kuboresha Mwongozo wa Maadili
ya Taifa na Utamaduni wa Mtanzania ili kulinusuru Taifa dhidi ya
mmomonyoko wa Maadili na utamaduni wan chi yetu kwa ujumla wake.
“Kitabu kinalenga kutoa mwongozo kwa jamii ya kitanzania kurejea katika
misingi yetu ya maadili kama Taifa kwa kupenda, kuthamini na kuheshimu
mila na desturi zetu ambazo ni miongoni mwa nguzo kuu za utamaduni
wetu”. Amefafanua Dkt. Temu.
Aidha, amesema kitabu hicho cha
Mwongozo kinazingatia Tamko la Sera ya Utamaduni la mwaka 1997, Sura ya
Pili, Kipengele cha Pili, Sehemu ya Tatu (2:2:3) kuwa tuna wajibu wa
kurithisha na kuendeleza Maadili, Mila, na Desturi Nzuri.
Pia,
Kitabu hicho kinakusudia kutoa mwelekeo na umuhimu wa kuzingatia maadili
kwa makundi mbalimbali ya jamii wakimemo wanafunzi katika ngazi
mbalimbali za elimu, vijana, watumishi wa umma na jamii kwa ujumla.
Akiwapitisha
wajumbe katika yaliyomo ya kitabu hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa
Utamaduni anayeshughulikia eneo la Lugha, Dkt. Resan Mnata amesema
kitabu hicho kina na jumla ya sura tano, ambapo sura ya Kwanza imejikita
katika Usuli; Sura ya Pili mmomonyoko wa maadili katika jamii; Sura
tatu wajibu wa makundi mbali mbali katika kukuza na kuendeleza Utamaduni
na maadili; Sura ya nne Usimamizi, uhifadhi, utekelezaji na uendelezaji
wa utamaduni na maadili na Sura ya tano mambo muhimu ya kuzingatia na
mapendekezo.
Akichangia katika kikao hicho, Mjumbe kutoka Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) Bi. Bona Leon, ameshauri baada ya kukamilika
kwa muongozo ni muhimu kukatengenezwa kitabu kidogo chenye lugha rahisi
kitakachosambazwa kwa jamii ili ujumbe uliokusudiwa uweza kuwafikia
watu wengi kwa urahisi.
Katibu Mkuu wa Habari, Dkt. Hassan
Abbasi katika Dibaji amesema kitabu hiki kinaeleza juhudi za Serikali
za kukuza na kujenga Maadili na Utamaduni wa Mtanzania ambapo amefafaniu
kwamba uhai na utambulisho wa Taifa lolote duniani, hutegemea utamaduni
wa Taifa husika.
“Kwa maneno mengine, utamaduni ni kielelezo na utambulisho wa Taifa na watu wake” Amehitimisha Dkt. Abbasi
Naye,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Lugha
Bashungwa kwenye kurasa wake wa ujumbe wa Mhe Waziri amesema anaamini
Kitabu hicho cha Muongozo kitatumika kama nyezo muhimu katika
kulirejesha Taifa kwenye misingi ya maadili ya taifa na utamaduni wa
mtanzania na kuwa kitasaidia kulinusuru Taifa la Tanzania kutoka katika
minyororo ya tamaduni za kigeni na kujenga moyo wa kuthamini, kudumisha
na kuendeleza Maadili mema kwa Jamii ya Watanzania wote.
Washirki wa kikao cha wadau kwa ajili ya kutoa maoni ya Mwongozo wa Maadili ya taifa na Utamaduni wa Mtanzania kilichofanyika leo Agosti 18, 2021 jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment