SERIKALI
imeutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma nchini PSSSF
kuendelea na mipango yake mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa umma katika
maeneo ya msingi kama vile uanachama na uchangiaji, ulipaji wa mafao na
mambo mengine muhimu ya kuzingatia wakiwa katika ajira, wakati wa
kustaafu na baada ya kustaafu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama wakati
akifunga semina za wastaafu watarajiwa zilizoandaliwa na PSSSF na
kufanyika Dar es Salaam.
Waziri Mhagama ameuelekeza mfuko huo
kuepusha usumbufu usio na lazima kwa wazee wanaodai mafao huku pia
akiwataka kuhifadhi taarifa zao vizuri na waziuishe kwa mara kwa mara
ili kuepusha ucheleweshaji wa mafao mwanachama anapostaafu.
Amesema
kwa upande wao kama Serikali wanaimani kwamba sekina hizo zitaleta tija
kwa wastaafu wote nchini ambapo ameongeza kuwa matarajio yao ni kuona
kwamba pensheni inamsaidia Mstaafu kuishi maisha bora kama ambavyo
alikua mtumishi.
"Nitoe wito kwa wastaafu mnapoamua kutumia mafao
yenu kuwekeza basi ni vema mfanye uwekezaji sahihi, uwekezaji makini na
pia muwekeze kwenye aina ya biashara mnayoielewa vema, mfano mtu
umefanya kazi muda mrefu Dodoma ni wazi ukiwekeza kwenye kilimo cha
Zabibu utakua unakielewa vema," Amesema Mhagama.
Ametoa wito pia
Kwa Menejimenti za Mabenki nchini kuangalia mifumo yao vema ili
kupunguza wimbi la matapeli ambao wamekua wakiwapigia simu wastaafu
wakiwa na taarifa zao na kisha kuwahadaa kutoa fedha.
" Naomba
Menejimenti za Mifuko na Wakuu wa Mabenki yetu leo tujiulize matapeli
hawa wanapatiwa taarifa na nani, je ni watumishi wetu wasiowaadilifu au
watu wengine humo kwenye Ofisi zetu tuliowaamini na kuwaacha waingie
popote?
Ninajiuliza uvujaji wa taarifa hizi unatoka wapi Kama
tatizo linaanzia kwa waajiri au mifumo yetu ya TEHAMA ni vema tujue na
kudhibiti ili kumaliza malalamiko haya," Amesema Waziri Mhagama.
Ameutaka
Mfuko wa PSSSF kuendelea na semina hizo mara kwa mara kwani kwa kufanya
hivyo watakua wanawatendea haki wanachama wao ambao wengi hawana elimu
ya kutosha ya usimamizi wa fedha na ubunifu wa miradi.
No comments:
Post a Comment