Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) na wafanyakazi wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), mara baada ya Naibu Waziri Ulega kufika katika ofisi hizo zilizopo Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam kushuhudia ukarabati wa miundombinu unaoendelea kufanywa katika jitihada za kufufua shirika hilo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amelitaka Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kujipanga kibiashara pamoja na kiubia na makampuni binafsi ya uwekezaji mara baada ya kufufuliwa na kuzinduliwa rasmi ili liwe na tija kwa wavuvi na taifa kwa ujumla.
Mhe. Ulega amesema hayo (10.08.2021) mara baada ya kufika katika ofisi za TAFICO zilizopo Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na kufafanua kuwa ni lazima uwepo mkakati na mbinu za kujielekeza zaidi katika uchumi wa bluu ili nchi ifaidike na rasilimali samaki na mazao yake na kuhakikisha uchumi wa wavuvi wadogo unakua ili shirika hilo liwe na tija zaidi.
Mhe. Ulega amemuelekeza Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya kusimamia mbinu na mkakati imara wa ufufuaji wa shirika na kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Prof. Mgaya ana uzoefu mkubwa kwenye sekta ya uvuvi na kwamba ataweka dira imara ya TAFICO katika mikakati ya kuhakikisha shirika linakuwa na tija kwenye sekta ya uvuvi hususan katika uvuvi wa bahari kuu.
“Hivi karibuni haitazidi miezi mitatu tunapokea meli ya uvuvi tunataka ikifika ianze kazi mara moja, meli ikute tumekaa kwenye mpango kazi iende kuvua samaki wa kutosha bahari kuu na ilete hao samaki kwa wingi wauzwe ndani na nje ya nchi.” Amefafanua Mhe. Ulega
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO Bi. Esther Mndeme amesema ukarabati unaendelea kufanywa katika miundombinu mbalimbali iliyopo kwenye eneo hilo baada ya serikali kufufua shirika hilo na kwamba baadhi ya miundombinu inahitaji ukarabati mkubwa na mingine kidogo kutokana na miundombinu hiyo kutofanya kazi kwa takriban miaka ishirini.
Bi. Mndeme amesema licha ya changamoto za kifedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ukarabati huo unafanyika kwa muda uliopangwa ili shirika lianze majukumu yake rasmi kama ambavyo imekusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya, amesema shirika likianza kufanya kazi vizuri litaleta tija katika uchumi wa bluu kwa kuwa fursa nyingi zitafunguka na taifa kupata tija zaidi kiuchumi na wavuvi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa amesema uwepo wa TAFICO katika wilaya hiyo kutaongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa upande wa ajira pamoja na kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Dar es Salaam kwa kujionea utendaji kazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na ukarabati wa majengo ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
No comments:
Post a Comment