Veronica Simba na Zuena Msuya - Manyara
Viongozi
mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato,
Wabunge wa Majimbo yaliyopo Wilaya ya Mbulu na Mkuu wa Wilaya hiyo,
Sezaria Makota, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Samia Suluhu kwa utekelezaji makini wa miradi ya umeme vijijini.
Walitoa
pongezi hizo kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi
wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa
wa Manyara, iliyofanyika Agosti 14 mwaka huu, kijiji cha Mongahay, Kata
ya Tumati, wilayani Mbulu.
Akizungumza na wananchi kabla ya
kuzindua rasmi Mradi huo, Naibu Waziri Byabato alisema kuwa Rais Samia,
kupitia Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza, amewezesha upatikanaji
wa fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha vijiji vyote ambavyo
havijafikishiwa umeme vinapelekewa nishati hiyo kabla ya Desemba 2022.
Byabato
alitumia jukwaa hilo kutoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa ya
kufikiwa na miundombinu ya umeme katika maeneo yao kwa kuhakikisha
wanalipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe na kuutumia katika
shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuboresha maisha yao.
“Mheshimiwa
Rais ametuwezesha tukawaletea umeme, niwaombe Waheshimiwa Wabunge
mhamasishe wananchi wenu wakimbilie fursa hii ili iwaletee maendeleo.”
Akifafanua,
Naibu Waziri alieleza kuwa katika baadhi ya maeneo ambayo yaefikishiwa
miundombinu ya umeme, mwitikio wa wananchi kulipia ili kuunganishiwa
nishati hiyo, umekuwa mdogo, jambo alilolielezea kuwa ni kurudisha nyuma
jitihada za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
“Serikali
inatumia gharama kubwa kuhakikisha miundombinu ya umeme inatufikia.
Sasa, miundombinu ikifika kwenye maeneo yetu, tuhakikishe sisi sote
tunahamasishana kuchangamkia fursa hiyo,” alisisitiza Naibu Waziri
Byabato.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Sezaria
Makota alipongeza kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu
ya Sita katika kusambaza umeme vijijini huku akitilia mkazo kuwa vijiji
vyote vya Wilaya hiyo, ambavyo havijafikiwa na umeme, vimeingia katika
kufikishiwa nishati hiyo kupitia Mradi huo uliozinduliwa siku hiyo.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mji, Zacharia Issaay alieleza kuwa kazi ya
kusambaza umeme vijijini iliyofanywa na Serikali kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) ni ya kupongezwa sana kwani imesaidia kwa kiasi
kikubwa kuboresha maisha ya wananchi.
“Nichukue nafasi hii
kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa kazi kubwa ya
usambazaji umeme vijijini kupitia REA.”
Mbunge Issaay
alibainisha kuwa kadri umeme unavyounganishwa katika maeneo mbalimbali
ndivyo wananchi wengi wanavyohamasika kufungua miradi ya kimaendeleo
zikiwemo mashine za kusaga nafaka, hivyo akaiomba Serikali kuongeza wigo
wa upelekaji huduma hiyo kwa manufaa ya jamii husika.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Fratei Massay
alimwomba Naibu Waziri Byabato kufikisha salamu za wananchi wa eneo hilo
alizoziita ‘za kindakindaki’ kwa Rais Samia kutokana na kazi kubwa
anayoifanya ya kuwapelekea maendeleo ikiwemo umeme.
“Naishukuru
Serikali kwenye Bajeti hii iliyopita, tumepata vijiji karibu vyote
kasoro kimoja tu. Ukikosa kimoja haulalamiki bali unashukuru,”
alisisitiza Masai.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos
Maganga alibainisha kuwa Mkoa wa Manyara una jumla ya vijiji 441 ambapo
vijiji 278 tayari vina umeme na vilivyosalia 163 vinapelekewa nishati
hiyo kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.
Kwa
upande wa Wilaya ya Mbulu, Mhandisi Maganga alieleza kuwa kuna jumla ya
vijiji 110 ambapo vyenye umeme ni 48. Alifafanua kuwa vijiji
vitakavyopelekewa umeme kupitia Mradi huo wa Awamu ya Pili ni 62 na kwa
gharama ya shilingi bilioni 18.8.
Mradi wa Kusambaza Umeme
Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kwa Mkoa wa Manyara unatekelezwa
na Kampuni ya Ukandarasi ya Nakuroi Investment pamoja na Giza Cable
Industries Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 65.3.
Naibu
Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akiwasha umeme katika Shule
ya Msingi Mongahay iliyopo Kata ya Tumati wilayani Mbulu, Mkoa wa
Manyara kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa huo. Tukio hilo lilifanyika
Agosti 14, 2021. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Sezaria Makota
(katikati), Mbunge wa Mbulu Vijijini, Fratei Massay (mwenye kofia) na
Mbunge wa Mbulu Mji, Zacharia Issaay (kulia).
Monday, August 16, 2021
RAIS SAMIA APONGEZWA UTEKELEZAJI MIRADI YA UMEME VIJIJINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment