HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 16, 2021

MWALIMU NA MWENZAKE MBARONI WAKITUHUMIWA KUMUUA MTOTO WA MIAKA MITANO KWA KIPIGO SINGIDA

 

Na Dotto Mwaibale, Singia

JESHI la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia Mwalimu   Regina Laurent, (28) wa Shule ya Msingi Mang'onyi na  Mathias Marmo  (30) kwa tuhuma za kumuua kwa kipigo mtoto mwenye umri wa miaka 5 aitwaye Joyce John, mkazi wa Kijiji na Kata ya Mang’onyi,  wilayani Ikungi mkoani hapa.

Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (  ACP) Stella Mutabihirwa  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa watuhumiwa hao walikuwa ni walezi wa mtoto huyo na kuwa uchunguzi zaidi ukikamilika wote wawiliwatafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalowakabili.

Mutabihirwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusu tukio hilo alisema Agosti 11/2021 majira ya saa 1:30 usiku katika Hospitali ya Malkia wa Ulimwengu iliyopo maeneo ya Puma, Wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida mtoto huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu hospitalini hapo ambapo wauguzi wa hospitali hiyo walitilia mashaka kifo hicho kutokana na majeraha aliyokuwa nayo marehemu na ndipo waliamua kutoa tarifa kwa Jeshi la Polisi.

Alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida lilipata taarifa hizo siku hiyo majira ya saa 2:00 usiku ambapo lilifanya uchunguzi wa awali na kubaini kuwa majeraha aliyoyapata marehemu yalitokana na kupigwa na vitu vinavyodhaniwa  kuwa ni fimbo na kitu butu sehemu mbalimbali za mwili wake na wazazi wake walezi ambao ni Mathias Marmo, (30), Mwalimu wa Shule ya Msingi Mang'onyi na Regina Laurent, (28), wote wairaq na wakazi wa mang'onyi.

Aidha Mutabihirwa alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alikuwa akipigwa na kufanyiwa ukatili mara kwa mara na walezi wake hao na kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kukemea vitendo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi wazazi na walezi na linawaomba wananchi kuachana na vitendo hivyo vikiwemo kutoa adhabu zisizokuwa na mipaka kwa watoto na kusababisha unyanyasaji wa kijinsia na wazazi wameaswa kuwalea watoto wao katika maadili mema.

Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (  ACP) Stella Mutabihirwa. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad