HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 5, 2021

ADAIWA KUMUUA MAMA YAKE KWA MADAI YA KUNYIMWA SHILINGI ELFU TANO

 

Na Mwandishi wetu, Hanang'

MKAZI wa Kijiji cha Measkron Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, John Ammi (24) anashikilia na polisi kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi Kasi Salai (50) kwa kumpiga na nyundo kichwani baada ya kumuomba shilingi elfu tano na kumnyima.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililotokea Agosti moja jioni, Salai ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Measkon alifariki dunia wakaati akikimbizwa hospitalini.

Shuhuda wa tukio hilo John Tluway akizungumza jana amesema Ammi baada ya kumuomba mama yake shilingi elfu tano na kunyimwa alinyang’anyana simu na mama yake ili akaiuze.

“Baada ya kushindwa kuchukua simu hiyo ili akaiuze alinyanyua nyundo na kumpiga nayo mama yake mzazi kichwani na kufariki dunia akikimbizwa hospitali ya Tumaini ya wilaya,” amesema Tluway.

Jirani wa marehemu huyo Hawa Raphael amesema siku mbili kabla ya tukio hilo mtoto huyo alichoma moto nguo za wazazi wake kwa sababu ya kunyimwa fedha za kunywa pombe.

“Mtoto huyo inasemekana alikuwa anavuta bangi na alikuwa na akili sana shuleni kwani alipata alifaulu kidato cha nne kwa kupata daraja la kwanza ila bangi zikamuharibu,” amesema.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) Marrison Mwakyoma, amethibitisha kukamatwa kwa Ammi kwa kudaiwa kumuua mama yake mzazi.

Kamanda Mwakyoma amesema Salai ni mkuu wa shule ya sekondari Measkon na Ammi ni mtoto wake wa kumzaa wanayeishi naye kwenye kijiji hicho cha Measkron.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni mwalimu huyo kuombwa fedha na mtoto wake wa kumzaa Ammi ili akafanye matumizi yake ya kujikimu akanyimwa kisha akamuua.

“Baada ya mtoto huyo kunyimwa fedha na mama yake alimpiga kichwani na kitu butu kisha mwalimu huyo akafariki dunia akipelekwa hospitali,” amesema Kamanda Mwakyoma.

Amesema polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kumfikisha mahakamani kujibu mashtaka hayo ya mauaji ya mama yake mzazi.

Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutojichukulia sheria mkononi na pindi kukitokea tatizo ni vyema kusuluhisha kuliko kusababisha mauaji kwani siyo suluhisho.

Mkuu wa shule ya sekondari Measkron Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, Kasi Salai (wapili kulia) akiwa na familia yake enzi za uhai wake, kabla ya kudaiwa kuuawa kwa kupigwa nyundo kichwani na mtoto wake John Ammi (kulia) baada ya kumnyima shilingi elfu 5.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad