HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 8, 2021

Benki ya CRDB yazindua programu ya mafunzo ya uongozi kwa wahitimu wa vyuo vikuu “Graduate Development Program”


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akiwapongeza wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamechaguliwa kushiriki programu ya mafunzo ya uongozi kwa wahitimu wa vyuo vikuu “Graduate Development” inayoendeshwa na Benki ya CRDB. Kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Siaphoro Kishimbo.
Benki ya CRDB imezindua program ya mafunzo ya uongozi kwa wahitimu wa vyuo vikuu “Graduate Development Program,” ambayo inalenga katika kuwaandaa wahitimu wa vyuo kuwa wabobevu katika masuala ya benki, na kuwajenga katika uongozi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika hoteli ya Serena, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB alisema programu hiyo itasaidia kujenga viongozi wa kesho wa benki hiyo na kuifanya kuendelea kuwa shindani katika soko nchini. 
“Benki yetu inakua kwa kasi sana kwa maana ya kupanuka kwa mtandao wa matawi nchini, lakini pia tupo Burundi na tupo katika mchakato wa kwenda Congo DRC. Ukuaji huu unatuhitaji sisi kama Benki kuandaa viongozi wa kesho na wafanyakazi ambao wataweza kuendana na mabadiliko katika soko,” aliongezea Nsekela.

Programu hii imezinduliwa kipindi muafaka ambacho Serikali na wadau wa maendeleo nchini wanawekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo vikuu nchini wanapata ajira na kutengenezewa mazingira ya kujiajiri.

“Leo hii tukiwa tunazindua programu hii, tayari tunao vijana 32, watatu kutoka Burundi, ambao wanapitia mafunzo haya ya Graduate Program. Vijana hawa wanapitishwa katika mafunzo ya hali juu katika matawi, idara na vitengo mbalimbali ndani ya Benki ili kuwajenga kuwa wabobevu, na baada ya miaka mitatu ya programu wanapata ajira kamili,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa programu hiyo ni moja ya jitihada za Benki ya CRDB kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu.
Akielezea mchakato uliotumika kuwapata wanafunzi hao, Mkurugenzi Rasilimali Watu Benki ya CRDB, Siaphoro Kishimbo amesema mwaka jana mwishoni benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya rasilimali watu ya Niajiri ilitangaza nafasi za mafunzo hayo ambapo wanafunzi wengi waliomba na kupitishwa katika mchakato wa usahili ambapo 32 walichaguliwa.

“Mpaka sasa ni miezi mitano tokea vijana hawa wajiunge katika program hii. Kama Benki tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la ajira kwa vijana,” alisema Kishimbo huku akibainisha kuwa baada ya miaka mitatu ya kuhitimu vijana wengine wanaohitimu vyuo vikuu wataajiriwa kupitia programu hiyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori aliwapongeza vijana ambao wamepata nafasi ya kushiriki programu hiyo huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi wa hali ya juu. 
“Nimeambiwa mmeanza vizuri sana na mmeshaanza kuwa wabobevu katika maeneo ya awali mliyopitishwa. Matarajio yetu ni kuwaona katika nafasi za uongozi baada ya miaka hii mitatu kama alivyoeleza Mkurugenzi Mtendaji,” alisisitiza Prof. Mori.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya washiriki wa program hiyo, Aurelia Haule aliushukuru uongozi wa Benki ya CRDB kwa kutoa fursa ya mafunzo na ajira kwa vijana. Alisema kwa kipindi cha miezi mitano ya walichojiunga na benki hiyo wamejifunza vitu vingi kuhusiana na uendeshaji na usimamizi wa benki. “Ni imani yangu kuwa baada ya programu hii tutakwenda kuwa wabobevu na kuisaidia benki yetu kupiga hatua kubwa kiutendaji,” aliongezea Aurelia.





















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad