Benki ya CRDB imewashukuru wateja na wadau wake kwa kuchaguliwa kuwa Benki bora nchini Tanzania kwa mara ya tatu mfululizo na jarida la kimataifa la Global Finance huku pia ikitajwa kuwa Benki inayoongoza kwa ubunifu. Benki ya CRDB imekuwa miongoni mwa benki 35 Afrika zilizotajwa kuwa bora na jarida hilo mashuhuri la nchini Marekani .
Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya benki hiyo mtaa wa Azikiwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliwahukuru wateja na wadau wa benki hiyo kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa mageuzi ya biashara (business transformation) ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kupata tuzo hiyo.
Aidha aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na mchango katika kuimarika kwa biashara nyingi ikiwamo sekta ya fedha. Nsekela alisema benki hiyo imeendelea kuunga mkono serikali katika jitihada zake za kuimarisha uchumi hususani katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Maradi wa Umeme wa Maji wa Nyerere (Stieglers).
Akizungumzia kuhusu tuzo ya ubunifu ambayo benki hiyo imetunikiwa, Nsekela alisema inatokana na huduma ya SimBanking mpya ambayo inawezesha wateja kufungua akaunti wenyewe (Self-Account Opening). Huduma hiyo imetambuliwa kama ubunifu wenye mchango mkubwa zaidi katika kuchochea ujumuishi wa kifedha nchini ‘financial inclusion.’
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya CRDB alisisitiza kuwa benki yake itaendelea kutilia mkazo katika kufikisha huduma kwa Watanzania wengi zaidi na kubuni huduma bunifu zinazokidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wateja na sekta mbambali za uchumi nchini.
Katika taarifa yake Mkurugenzi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Global Finance, Joseph Giarraputo, mchapishaji na mkurugenzi wa uhariri wa Global Finance alisema washindi tuzo za mwaka 2021 ni zile benki ambazo zilijikita katika kuwawezesha wateja kuvuka changamoto zilizosababishwa na corona na kuimarisha uchumi. Aidha alisema Jarida hilo pia limetazama matokeo ya kifedha kwa mwaka 2020.
"Benki ya CRDB imekuwa na mchango mkubwa kwa wateja na uchumi mwaka 2020. Ama hakika ilidhihirisha kuwa ni benki kiongozi kwa namna ambavyo ilikidhi mahitaji ya wateja na jamii kwa katikati ya changamoto. Pamoja na kujitoa kwao, wameweza tumeshuhudia ukuaji mkubwa katika biashara yao" alisema Giarraputo.
Katika orodha kamili iliotolewa karibuni na Jarida la Global Finance, kundi la majaji lilifanya upembuzi kwa benki zilizopo kwenye nchi 150 duniani kote. Benki ya CRDB imetunukiwa kwa upande wa Tanzania, ikungana na benki nyengine tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.
Jarida la Global Finance linachapishwa na GFMag.com mtandao wa kuaminika katika upembuzi wa mahesabu na uwekezaji la New York, nchini Marekani.
No comments:
Post a Comment