Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMLA ya wanachama 900 wamesajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wananchi 2,500 wamepata huduma ya elimu ya umuhimu wa bima ya afya katika Maonesho ya SabaSaba tangu yaanze Juni 28 mwaka huu.
NHIF inashiriki maonesho hayo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam ambapo huduma mbalimbali zinatolewa ikiwemo ya elimu, usajili wa wanachama pamoja na kupokea maoni na kutatua changamoto zinazowakabili wanachama.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi kufika bandani hapo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Bi. Anjela Mziray amesema kuwa, wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kufika na kupata huduma za elimu na kujiunga ili wanufaike na mafao yanayotolewa.
“Tangu maonesho haya yaanze tumeshahudumia zaidi ya wananchi 2,500 kwa kuwapatia elimu na tumesajili jumla ya wanachama wapya 900 wakiwemo watoto chini ya umri wa miaka 18 na waliojiunga kupitia mpango wa vifurushi,” alisema Bi. Mziray.
Alisema kuwa Mfuko umejipanga kuwahudumia wananchi hivyo wajitokeze na wafike katika banda la Mfuko ambalo liko nyuma ya banda la Jakaya Kikwete. “Tuko hapa mpaka Julai 13, mwaka huu hivyo wananchi watumie fursa hii kufika na kujiunga.
Maafisa wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) wakiwa wanendelea na kazi ya kusajili wananchi wanaojitokeza kupata huduma ya bima ya Afya katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa mkoa wa Dar es Salaam.
Wananchi wakiendelea kupata huduma ya Bima ya Afya katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) leo katika maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment