Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Moshi
Serikali imeonyesha kutoridhishwa na muenendo wa chama kikuu cha ushirika Mkoani Kilimanjaro (KNCU) ambapo wanachama wametakiwa kusimama imara wakati wa uchaguzi katika kuhakikisha wanapatikana viongozi bora ambao wataiwezesha KNCU kusonga mbele.
Taarifa
ya tume ya waziri Mkuu kuhusu KNCU imebainisha madudu mengi ambapo
baadhi ya mali mbalimbali zilihujumiwa na nyingine kuuzwa ikiwemo
kuingiwa kwa mikataba isiyo sahihi.
Kati
ya vyama vya ushirika 43 vilivyofanyiwa ukaguzi na shirika la ukaguzi
wa mahesabu kwa vyama vya ushirika (COASCO), vyama 12 vimepata hati
zisizoridhisha jambo ambalo halileti taswira nzuri.
Waziri
wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 28 Juni 2021
wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 36 wa chama kikuu cha ushirika
Mkoani Kilimanjaro (KNCU) ambapo amesisitiza kuwa serikali inahitaji
sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili kuiwezesha kuleta tija kwenye
ushirika.
Amesema
kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria ya
vyama vya ushirika ya mwaka 2013 lengo likiwa ni kuondoa madhaifu
yanayodidimiza vyama hivyo nchini.
Waziri
Mkenda amewataka wanaushirika kuipitia sheria hiyo na kutoa maoni
ambayo yatawezesha kuiboresha sheria hiyo na kuifanya kuwa na tija
katika vyama vya ushirika nchini.
"Ingekuwa
ni mamlaka yangu ningesema viongozi wote wa bodi waondoke na msigombe
na tuchague wengine ila kwasababu ushirika ni mali ya wanaushirika
niwaombe mtumie nafasi yenu kuhakikisha mnawashawishi wale wenye uwezo
kugombe nafasi za uongozi" Amesema Waziri Mkenda na kuongeza kuwa
"Kwa
hali hii naona vyama vya ushirika vishindane katika kupata hati safi
maana ni lazima hesabu zipangwe vizuri maana mali bila daftari huisha
bila habari"
Aidha,
Prof Mkenda aliutaka umoja wa vyama 32 vya ushirika (G32) kufuata
sheria kama wanavyopewa maelekezo na Mrajisi wa vyama vya ushirika
nchini, katika kuanza kufanya biashara ya kahawa na kwamba iwapo
watashidwa kufuata sheria serikali haitakuwa radhi nao.
Akizungumza
katika mkutano huu, Mrajisi wa Taifa wa vyama vya ushirika, Dkk Benson
Ndiege, amesema mkutano Mkuu wa uchaguzi wa KNCU uliahirishwa kwa lengo
la kutoa frusa kwa wanachama kuchagua viongozi Bora ambao watakuwa na
uwezo na ubunifu.
"Tatizo
kubwa linalokabili vyama vya ushirika hapa nchini ikiwa ni pamoja na
KNCU Ni kukosekana kwa dhana ya utawala bora, mkutano wa uchaguzi
umeahirishwa tumieni nafasi hii kupata viongozi ambao wataitoa KNCU
ilipo na kuisogeza mbele kwa manufaa ya wakulia" Amesema
Naye
Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Kahama (KNCU), Emanuel
Cherehani, amesema ili KNCU ifanikiwe ni lazima viongozi kuwa waaminifu,
waadilifu pamoja wabunifu ili kusaidia chama hicho kupiga hatua zaidi
na wakulima kuona mchango wake.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania-SAGCOT, Ndg Geoffrey Kirenga amesema kuwa KNCU ina nafasi kubwa kurudisha heshima ya Ushirika Tanzania.
No comments:
Post a Comment