TIRA yaipongeza Benki ya CRDB uzinduzi wa kampeni maalum ya elimu ya Bima kwa Umma - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 16, 2021

TIRA yaipongeza Benki ya CRDB uzinduzi wa kampeni maalum ya elimu ya Bima kwa Umma

Dar es Salaam 15 Juni 2021 – Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (TIRA) imeipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa kampeni maalum ya elimu ya bima kwa umma. Akitoa salamu za pongezi kwaniaba ya Kamishna wa TIRA wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency, Mkurugenzi wa Ukuzaji Masoko, Utafiti na Mipango wa TIRA, Zakaria Muyengi alisema kampeni hiyo itasaidia kufikia lengo la Serikali la kuongeza ujumuishi wa bima nchini.

Muyengi alisema katika Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka 10 2020/2021 hadi 2029/2030 ambao ulizinduliwa mwezi Septemba mwaka jana Serikali imeka lengo la kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo huduma za bima. 

“Takwimu zinaonyesha ni asilimia 15 tu ya Watanzania wote ndio wanatumia huduma za bima ambapo ni kiwango kidogo sana ikilinganishwa na nchi kama Afrika Kusini. Lengo ni ifikapo mwaka 2034 tuongeze kiwango cha ujumuishi wa bima kufikia asilimia 50 ya Watanzania,” alisema Muyengi huku akibainisha kuwa mpango huo pia una lenga kuongeza mchango wa sekta ndogo ya bima katika Pato la Taifa kutoka asilimia 1 hadi asilimia 3.Akizungumzia mkakati wa Serikali katika ufikishaji wa huduma za Bima kwa Wananchi, Muyengi amesema TIRA inaendelea kuhakikisha sheria ya utekelezaji wa mfumo wa utoaji huduma za bima kupitia benki “BancAssurance” inatekelezwa kikamilifu. Muyengi alisema mfumo wa BancAssurance unasaidia kujibu changamoto nyingi zilizokuwa zikisababisha watu wengi kuwa nje ya mfumo wa bima, huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa moja ya Benki zilizojiunga na mfumo huo.

“Nafahamu Benki ya CRDB mnauzoefu mkubwa katika huduma za bima kulinganisha na wengine, kwani nyie mlianza na kampuni ya udalali ambayo imekuwa ikifanya vizuri. Tumieni uzoefu huo kuboresha zaidi kwa maana ya kuja na bidhaa na njia bunifu za ufikishaji huduma za bima kwa kushirikiana na makampuni ya bim,” aliongezea Muyengi huku akipongeza ubunifu wa huduma za bima za KAVA Assurance na Bima ya Vyombo vya Moto kidijitali kupitia SimBanking zinazotolewa na Benki ya CRDB na makampuni washirika ya bima.

Akizungumzia kuhusu suala la elimu ya bima kwa umma, Muyengi alisema Serikali kupitia Sheria ya Bima imeelekeza kuwa taasisi zote zinazotoa huduma za bima zinapaswa kuhakikisha wafanyakazi wake wanaohusika kutoa huduma hizo wanapata mafunzo ya mara kwa mara, kuwasilisha mpango wa elimu ya bima kwa umma na kutenga bajeti ya utekelezaji. 

 “Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kutimiza takwa hili la kisheria, mpango wenu wa elimu ya bima kwa umma tumeupokea na kuupitisha na leo hii mmetuita kuja kuona jinsi mnavyokwenda kutekeleza kwa vitendo, hongereni sana,” alipongeza Muyengi huku akiitaka Benki ya CRDB kutoishia kutoa elimu hiyo katika matawi na kwenda mpaka kwa wananchi kupitia makongamano ya elimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema dhumuni la kampeni hiyo iliyopewa jina la “Furahia Maisha, Bima Unachokithamini” ni kukuza uelewa wa masuala ya bima na kuhakikisha Wananchi wengi zaidi wanapata uelewa wa huduma hizo na hivyo kuhamasika kutumia katika kujikinga na majanga katika shuguli na maeneo mbalimbali katika maisha yao.  

“Tukiwa Benki ya kizalendo tunaamini tunawajibika katika kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunafikia ujumuisha wa bima kwa asilimia 50 kama ambavyo imeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha,” alisema Nsekela ambapo alisisitiza kuwa kuskosekana kwa elimu ni moja ya sababu kubwa ya kuwa na matumizi madogo ya bima nchini.

Nsekela alisema kupitia kampeni hiyo Benki ya CRDB imejipanga kutoa elimu ya bima kupitia warsha za elimu ambao zitaendeshwa na Benki hiyo nchi nzima, vilevile Benki hiyo imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu hiyo inafika kila kona ya nchi. 

“Hivi karibuni pia tutakwenda kutazindua kampeni yetu ya Tupo Mtaani Kwako kwa mwaka 2021, kampeni hii pia itahusisha elimu ya bima. Hivyo niwaombe Watanzania wanapowaona wafanyakazi wetu mtaani wasisite kuuliza maswali kwani sisi tumejipanga kikamilifu kuwapa elimu ya bidhaa zetu ikiwamo bima,” aliongezea Nsekela.

Akielezea juu ya huduma za bima zinazopatikana katika Benki hiyo, Nsekela alisema bima hizo ni pamoja na bima ya vyombo ya vyombo vya moto, bima ya majengo na vitu vya ndani, bima ya moto, bima ya maisha, bima ya safari na bima ya afya. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad