Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
SERIKALI imesema imejipanga kisera na kutoa huduma muhimu na sheria rafiki zinazokidhi na kuvutia wawekezaji wa nje na ndani ya nje ya nchi ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndani ya bara la Afrika na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo wakati akizindua kongamano la uhusiano baina ya maeneo maalumu ya uwekezaji na uchumi wa ndani lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Tanzania (Uongozi Institute,) pamoja na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA,) na kuwakutanisha wawekezaji wa ndani na nje na kujadili namna ya kuunganisha maeneo muhimu ya uwekezaji na uchumi wa ndani pamoja na kuangalia namna ya kushirikisha wawekezaji wa ndani hasa wajasiriamali.
prof. Mkumbo amesema, katika kuhakikisha uchumi wa nchi unashindana kimataifa Serikali na taifa kwa ujumla linaendelea kujiunga na jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa ili kushindana kimataifa kama ilivyoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan juu ya msingi wa kuimarisha biashara ndani ya Afrika na nje ya mipaka kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wa taifa.
''Serikali imejipanga kisera, huduma muhimu katika maeneo ya uwekezaji, skills muhimu katika elimu ili kwenda na matakwa ya soko kwa ujumla pamoja na sheria za kodi katika kuhakikisha uwepo wa uzalishaji wenye tija katika maeneo ya viwanda.'' Amesema.
Aidha amesema, Serikali imejipanga Katika ujenzi wa mitaa ya viwanda "Industrial parts" pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo ya uwekezaj ya Kurasini, Bagamoyo na Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam.
Kwa upande wake kaimu mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA,) John Mnali amesema mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu katika maeneo ya uwekezaji kwa niaba ya Serikali kwa kuhakikisha maeneo yote ya uwekezaji yanapata huduma muhimu hasa miundombinu ya maji, umeme na barabara pamoja na kutoa leseni za uwekezaji kwa wawekezaji hao.
Amesema, wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya viwanda na biashara pamoja na wadau wengine wa uwekezaji kwa kuhakikisha wanayafikia mafanikio kwa kiwango kikubwa na hadi sasa wamesajili kampuni zipatazo 176 zenye uwekezaji wa dola za kimarekani bilioni 2.5 na watanzania 58198 wamenufaika kwa kupata ajira za moja kwa moja hadi kufikia Machi, 2021.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi (Uongoz Institute,) kwa kushirikiana na EPZA liliwakutanisha wawakilishi wa Serikali za mitaa, wawakilishi wa biashara ndogondogo na kati, kampuni za uwekezaji, Taasisi za Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara.
No comments:
Post a Comment