Charles James, Michuzi TV
KATIKA
kupunguza wimbi la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini,
Serikali imetoa wito kwa watanzania kujenga tabia ya kuasili watoto
kwani pia kufanya hivyo ni kujiongezea baraka mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wito
huo umetolewa leo jijini Dodoma na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango
wakati akizindua Makao ya Taifa ya Watoto katika eneo la Kikombo tukio
ambalo limeenda sambamba na siku ya mtoto wa Afrika.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais Dk Mpango amesema ni vema jamii
ikajijengea tabia ya kuasili watoto ili kuweza kupunguza wimbi la watoto
wanaoishi mtaani ambao hujikuta wakizama katika changamoto ya kutumia
dawa za kulevya na wengine kuingia kwenye biashara haramu.
Makamu
wa Rais Dk Mpango ameitaka pia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tamisemi kusimamia
huduma katika makao ya watoto ili yaweze kutolewa kwa sheria na
taratibu zilizowekwa pamoja na takwa husika.
" Nitumie fursa hii
kuwapongeza na kulishukuru Shirika hili la Abbott Fund kwa kutoa kiasi
kikubwa cha fedha kusaidia ujenzi wa kituo hiki ambacho kinakwenda kuwa
msaada kwa watoto wa Taifa hili.
Ni maelekezo yangu kwa Wizara za
Afya na Tamisemi kuhakikisha makao ya watoto hayaanzishwi kiholela
lakini pia kuhakikisha kwenye haya Makao kunakuepo na walezi wenye sifa
zinazofaa katika kuwahudumia watoto wetu," Amesema Dk Mpango.
Ameongeza
kuwa ni wajibu wa Wizara ya Afya na Tamisemi kuhakikisha inafuatilia
maendeleo ya vituo hivyo ili kuweza kujua nini kinafanyika sambamba na
kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili ya Kitanzania.
"
Wizara zinapaswa kufuatilia maendeleo ya makao haya ya watoto,
ufuatiliaji utatufanya tujue misaada inayotolewa na washirika wetu
wakiwemo Abbott Fund.
Ni vema pia tuhakikishe watoto wetu hawa
wanalelewa kwenye maadili yetu watanzania, kuna kituo kimoja
nilitembelea badala ya watoto kucheza ngoma za Kigogo walikua wanacheza
nyimbo za kihindi, Ni rai yangu kwenu kwamba watoto wetu hawa wanapaswa
kulelewa katika maadili, mila na tamaduni zetu watanzania," Amesema
Makamu wa Rais Dk Mpango.
Kwa upande wake Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema
kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ya Mtoto wa Afrika ni "Tutekeleze
Ajenda 2040: Kwa Afrika inayolinda haki za Mtoto" ambapo ajenda 2040 ni
matokeo ya mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika waliokutana nchini
Ethiopia mwaka 2015 na kutathmini hali ya utoaji wa haki za watoto
barani Afrika ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 25 ya utekelezaji
wa Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa mtoto wa mwaka 1991.
"Ajenda
2040 inahimiza masuala mbalimbali yakiwemo ya utekelezaji wa Mkataba wa
Afrika wa Haki na Ustawi wa mtoto wa mwaka 1991 kwa vitendo, kuweka
mfumo rafiki wa sera na sheria kuhusu haki za mtoto pamoja na kuwezesha
watoto kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Kuimarisha huduma
za malezi na makuzi ya mtoto, kuhakikisha kila mtoto anapata elimu,
kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili na kuhakikisha
watoto wanapata fursa ya kushiriki katika masuala yanayowahusu," Amesema
Dk Gwajima.
Nae Mkurugenzi wa Abbott Fund Nchini, Natalia Lebou
ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mkakati wa kuhakikisha inalinda
haki ya mtoto ambapo ameahidi Shirika lake kuendelea kushirikiana na
Serikali katika kulinda haki na ustawi wa watoto.
Lebou amesema
mradi huo wa Makao ya Taifa ya Watoto umegharimu kiasi cha Sh Bilioni 12
za Kitanzania ambapo pamoja na makazi ya watoto hao kuna miradi
mbalimbali ikiwemo Zahanati, Karakana, Maktaba ya kujisomea, bustani ya
mbogamboga na viwanja vya michezo na burudani.
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akizungumza katika uzinduzi wa Makao ya Taifa ya Mtoto katika eneo la Kikombo jijini Dodoma ambapo pia tukio hilo lilienda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akizungumza katika uzinduzi wa Makao Makuu ya Taifa ya Mtoto jijini Dodoma leo.
Mkurugenzi wa Shirika la Abbott Fund ambao ndio wafadhili wa Ujenzi wa kituo cha Makao ya Taifa ya Mtoto, Natalia Lebou akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Dodoma leo.
Muonekano wa juu wa Makao ya Taifa ya Mtoto yaliyojengwa jijini Dodom.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Afya na Naibu wake pamoja na baadhi ya watoto wanaolelewa kwenye kituo cha Makao ya Taifa ya Mtoto katika eneo la Kikombo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment