Na Adili Mhina
Tume
ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewapongeza walimu wa Wilaya ya Mwanga kwa
kuendelea kufanya kazi kwa weledi na nidhamu licha ya changamoto
mbalimbali zinazowakabili.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa
wiki na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya walimu
kutoka TSC, Christina Hape alipofanya ziara wilayani hapo kwa lengo la
kukutana na kuzungumza na walimu juu ya masuala mbalimbali ya
kiutumishi.
Hape alieleza kuwa TSC inatambua changamoto
mbalimbali za wilaya hiyo ikiwemo upungufu wa walimu pamoja na shule
nyingi kuwa maeneo ya mbali ambapo miundombinu na huduma mbalimbali bado
hazijafika.
Aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, walimu wa
wilaya hiyo wamekuwa mfano wa kuigwa kutokana moyo wa kufanya kazi kwa
bidii na kwa nidhamu, kitu kinachofanya Mkoa wa Kilimanjaro kuendelea
kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kitaaluma.
“Kwa kweli
Mwanga mnajitahidi kufanya vizuri, tunatambua kuwa yapo maeneo ya
milimani ambayo hata kufikika kwake ni changamoto. Nimeelezwa kuwa hata
kufika hapa kwenye mkutano huu wapo baadhi yenu mliolala kwenye magari
ili muweze kuwahi”, alisema Hape.
Aliongeza kuwa, “pamoja na
changamoto hizo mmeendelea kufanya kazi kwa kujituma na kwakweli hata
kule makao makuu hatujapokea rufaa nyingi zinazohusu utovu wa nidhamu
kwa walimu wa mwanga, naomba niwapongeze sana kwa hilo.”
Mkurugenzi
Hape alifafanua kuwa, suala la upungufu wa walimu sio la wilaya hiyo
peke yake bali maeneo mengi ya nchi kuna upungufu wa walimu na tayari
serikali imeamua kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na tatizo
hilo.
“Mtakumbuka kuwa hivi karibuni Rais wetu mpendwa Mama
Samia Suluhu Hassan alizungumzia suala la upungufu wa walimu na kuagiza
suala hilo tulishughulikie kwa haraka. Vilevile, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu naye
amesisitiza kuwa hataki kuona shule yenye walimu wawili au watatu,”
alisema Hape.
Aliongeza kuwa maagizo ya viongozi hao kuhusu
kutatua changamoto ya upungufu wa walimu inaifanya TSC pamoja na mamlaka
nyingine zinazohusika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha walimu
wanaajiriwa ili kujaza maeneo yenye upungufu.
Pamoja na hayo,
Mkurugenzi huyo alipongeza ushirikiano uliopo kati ya ofisi ya TSC
wilaya pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya
ya Mwanga na kusema kuwa ushirikiano huo ndiyo unaofanya walimu wafanye
kazi kwa moyo, nidhamu na weledi.
“Nishukuru ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji pamoja na ofisi ya TSC wilaya kwa kuwa mnafanya kazi kama timu
moja, hakuna mivutano. Kaimu Katibu wa TSC, Maafisa Elimu pamoja na
Maafisa Utumishi mnazungumza lugha moja katika kutatua kero za walimu.
Hii imefanya hata katika masuala ya kupandisha madaraja sijasikia
malalamiko kuwa kuna mwalimu amesahaukika,” alisema Hape.
Akitoa
taarifa fupi ya utendaji wa TSC wilayani hapo, Kaimu Katibu Msaidizi wa
TSC wilaya ya Mwanga, Catherine Kimaro alisema kuwa, wilaya hiyo ina
jumla ya walimu 1120 wanaofundisha shule za Serikali. Katika idadi hiyo,
walimu 558 ni wa shule za msingi na 562 ni wa shule za sekondari.
Kimaro
alieleza kuwa, wilaya hiyo kwa sasa haina shauri lolote la nidhamu
kutokana juhudi za ofisi yake za kutoa elimu kwa walimu mara kwa mara
kuhusu miiko na maadili ya utendaji wa kazi.
Monday, April 12, 2021
WALIMU MWANGA WAPONGEZWA KWA KUFANYA KAZI KWA NIDHAMU NA WELEDI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment