Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imerejesha
shamba la mjane wa Profesa Joshua Doriye aliyetaka kudhulumiwa na
viongozi wa Kijiji cha Getanuwas Wilayani Hanang’.
Mkuu wa
TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi
wa habari mjini Babati amesema mjane huyo wa Profesa Doriye aliyekuwa
Katibu Mkuu ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa wakati huo, alitaka
kudhulumiwa shamba hilo na Mwenyekiti wa kijiji hicho Adam Maulid
Mwanga.
Makungu amesema Profesa Doriye katika uhai wake kama
ilivyo kwa watanzania wengine alikuwa na haki ya kumiliki mali ikiwa ni
haki ya kikatiba iliyoainishwa chini ya ibara ya 24 (1) (2) katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomeka pamoja na
madhumuni ya kutungwa kwa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba
11/2007.
Amesema kati ya mali alizofanikiwa kumiliki wakati wa
uhai wake ni pamoja na shamba lilillopo kijiji cha Getanuwas wilayani
Hanang’ mkoani Manyara.
“Mwaka 2019 mjane wa marehemu huyo
Profesa Doriye wakati akishuhulikia shughuli ya mirathi Mwenyekiti wa
Serikali ya Kijiji cha Getanuwas Adam Maulid Mwangu kwa kushirikiana na
watu wengine waliokuwa na nia ovu ya kutwaa shamba hilo alikataa
kutambua umiliki wa ardhi wa marehemu Profesa Doriye katika kjiji hicho
hivyo kukwamisha ufungaji wa shauri la mirathi namba 47/2019 uliokuwa
ukiendelea mahakama ya mwanzo Kawe.
“Baada ya Mwenyekiti huyo
kutotambua umiliki huo mjane aliwasilisha malalamiko yake TAKUKURU na
tukaanzisha uchunguzi wa kina wa mjane huyo wa Profesa Doriye,” amesema
Makungu.
Amesema uchunguzi wao umebaini kwamba marehemu Profesa
Doriye alipewa shamba hilo na serikali ya kijiji cha Getanuwas tangu
mwaka 1978 na umiliki wake haukuwahi kuangaliwa na mtu yeyote katika
kipindi chochote na nyaraka zote kuhusu umiliki zipo na viongozi wa
wakati huo wamethibitisha pasipo shaka umiliki wa shamba hilo kwa
Profesa Doriye.
“Tulipomuhoji Mwenyekiti huyo wa kijiji wa sasa
Adam Maulid Mwangu kupitia ushahidi wa nyaraka mbalimbali alionyesha
kujutia kitendo alichomfanyia mjane, aliomba msamaha akieleza kwamba
yeye hakuwahi kuziona nyaraka za umiliki wa shamba hilo na hivyo kukiri
kumtambua mmiliki na kukiri kutomsumbua tena mjane na wanufaika wa
shamba hilo,” amesema Makungu.
Amesema shamba hilo pamoja na
nyaraka walikabidhi rasmi kwa mjane wa marehemu ili aweze kuendelea na
utaratibu wa kufunga mirathi hiyo katika mahakama ya mwanzo Kawe.
“Tunawaonya
baadhi ya wenyeviti wa vijiji wachache wa aina ya Adam Maulid Mwangu
kuwa hawakuchaguliwa kwenda kutegua maamuzi halali yaliyoamuliwa na
vikao halali vya serikali za vijiji zilizotangulia hasa katika eneo hili
la ardhi, kufanya hivyo kama alivyofanya Mwangu kwa nia ya kujipatia
ardhi ni matumizi mabaya ya madaraka na kinyume cha kifungu cha 31
sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2017 na watakaobainika
sharia itachukua mkondo wake,” amesema Makungu.
Alitumia nafasi
hiyo kuwafahamisha wana Manyara na watanzania kwa ujumla kwamba ukisoma
madhumuni ya kutungwa kwa sheria ya kuzuia na kupamba na rushwa namba
11/2007 yameainishwa kwamba sheria hiyo imetungwa ili kuhakikisha kuwa
wanaondokana na rushwa na dhuluma za aina zote na sheria hiyo imetungwa
ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anakuwa na haki ya kumiliki mali
aliyoipata kwa njia halali na umiliki huo utalindwa kwa msingi wa sheria
kama ilivyofanyika kwa mali ya marehemu Profesa Doriye.
“Hivyo
tunaendelea kuchukua hatua kwa wale wachache ambao kwa tamaa zao
wanagombea nafasi za kisiasa zikiwemo uenyekiti wa mtaa na vijiji kwa
nia ovu ya kwenda kupora mali za wananchi zilizopatikana kwa njia
halali,’’ amesema Makungu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati.
Monday, April 12, 2021
TAKUKURU MANYARA YAREJESHA SHAMBA LA URITHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment