HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 8, 2021

ML 700 ZAMALIZA KERO YA MAJI KIPAPA NA MHILO


 MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa),imekamilisha ujenzi wa miradi miwili ya  maji kwa mafanikio makubwa katika vijiji  vya Mhilo na Kipapa katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.


Kukamilika kwa miradi hiyo kumemaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa  maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji hivyo ambao kabla ya  ujenzi wa miradi hiyo, walilazimika kutumia maji ya visima vya asili vilivyochimbwa kienyeji na wengine kwenda mtoni kuchota maji  ambayo hayakuwa safi na salama.


Meneja ufundi wa Souwasa Jafari Yahaya alisema, Serikali imetoa  jumla ya shilingi milioni 772 ili  kujenga miradi  yote mwili iliyohusisha ujenzi wa  matenki, miundombinu mbalimbali na vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa katika makazi ya watu na kwenye taasisi za umma.


Akizungumzia mradi wa Kipapa Jafari alisema, serikali kupitia wizara ya maji  imetoa  shilingi milioni 569 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu  na kuboresha  huduma ya maji  ambapo kati ya hizo, tayari imetoa  milioni 444  kwa ajili ya kutekeleza  mradi huo.


Alisema, kazi zilizopangwa na zilizofanyika  ni ujenzi wa chanzo,ujenzi wa tenki la kusambazaji maji,usambazaji wa bomba za kusafirishia na kusambaza maji na kujenga vituo 23 vya kuchotea maji.


Kwa mujibu wake,kazi zimekamilika kwa asilimia 98 na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama,  isipokuwa  ujenzi wa uzio ambao  hajakamilika na unaendelea kujengwa.


Aidha katika mradi wa Muhilo  Jafari alisema, Serikali  imetoa  shilingi milioni 203  na kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki wa lita 50,000 na shughuli nyingine ambapo wakazi  1,247 wamenufaika na mradi huo.


Aliongeza kuwa, serikali imetoa fedha hizo kwa ajili ya  kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo ili watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo, badala ya kupoteza  muda wao kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.


Alisema, miradi yote  ipo chini  ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) mkoa wa Ruvuma na Souwasa ilipewa kazi ya kujenga kama fundi.


Jafari alisema, miradi yote imekamilika kwa asilimia 98  na sasa  wananchi  wanapata huduma ya maji katika maeneo yao pamoja na taasisi za serikali kama shule na zahanati na kuishukuru Ruwasa kwa kwa kuwaamini na kuwapa  kazi ya Ujenzi wa miradi hiyo.


Manfred Nchimbi(56) mkazi  wa Kipapa alisema, awali walilazimika kuamka saa 9 usiku na kutembea umbali wa km 3 kwenda kutafuta maji,  lakini sasa  kero hiyo imemalizika na kuishukuru serikali kupitia wizara ya maji kutekeleza mradi huo ambao umemaliza kabisa mateso  ya muda mrefu.


Alisema, kabla ya kujengwa kwa mradi huo na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) chini ya fundi Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa) walitumia maji kutoka katika vyanzo visivyo rasmi lakini  havikutosheleza mahitaji yao.


Kanisia Komba  mkazi wa kijiji cha Mhilo,mbali  na kuishukuru serikali kwa kupeleka huduma  ya maji katika kijiji  hicho alisema, maji  hayo yamerudisha na kuboresha mahusiano na kuimarika ndoa zao.

Alisema, baadhi ya ndoa zimevunjika kwa sababu ya akina mama kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji,  hivyo wanaume kudhani  walikuwa kwenye michepuko(nyumba ndogo) jambo ambalo lilichangia ndoa nyingi kuvunjika na  kusambaratika kwa familia.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad