HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 16, 2021

MKOA WA TANGA WAPOKEA JUMLA YA SH BILIONI 73 KWA AJILI YA MIRADI YA ELIMU NDANI YA KIPINDI CHA MIAKA MITANO

 


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Mkoa wa Tanga umepaokea jumla ya Sh bilioni 73 na milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu.

Makamu wa Rais amesema hayo Wilayani Korogwe Mkoani Tanga  wakati  akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Chuo cha  VETA Korogwe  ambapo amesema ahadi ya Serikali ni  kuendelea kuwasomesha watoto wa kitanzania kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne bila malipo pamoja na kujenga shule za sekondari,  Vyuo vya Ufundi na Vyuo Vikuu vya kutosha.

Amesema ameridhishwa na miradi ya Serikali inayotokelezwa katika mkoa wa Tanga ikiwepo ujenzi wa VETA mpya katika halmashauri  ya Korogwe na kutaka ikamilike kwa wakati ili iweze  kutoa elimu na ujuzi kwa vijana katika  Mkoa wa Tanga.

"Tanga inakua kwa viwanda vinavyojengwa na vitahitaji wataalamu, hivyo VETA Korogwe ikikamilika ichukue vijana ili tupate wataalamu watakaofanya kazi kwenye viwanda,"amesisitiza Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassa .

Nae Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema  Chuo cha Ufundi VETA  Korogwe ni moja kati ya Vyuo vya  vya ufundi 25 vinavyojengwa katika halmashauri mbalimbali nchini  kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Ujuzi na Kazi ambapo Serikali ilitenga Sh bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo na kwamba ujenzi wake  unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA.

Amesema sambamba na kujenga VETA hizo  bado zipo VETA nne ambazo zinajengwa kupitia Halmashauri ambazo ni Ruangwa, Kasulu Kongwa na Nyasa na kufanya VETA zinazojengwa kufikia 29 na kwamba zitakuwa zimekamilika kufikia Juni 2021 na kuanza kudahili.

 "Baada ya VETA hizi kukamilika, Mwezi Julai 2021 tunatarajia kudahili wanafunzi ambapo tutaongeza udahili wa wanafunzi elfu 24 mia sita na hamsini," Amesema Waziri Ndalichako.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa Kasongwa  amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia Chuo cha Ufundi VETA Korogwe  kwa kuwa kitataoa fursa kwa vijana  wa Halmashauri ya Korogwe na Tanga kwa ujumla kupata ujuzi na Maarifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dk Pancras Bujulu  amesema ujenzi wa VETA Korogwe  umefikia asilimia 65 ambapo mpaka kukamilika utagharimu  Sh bilioni 1 na milioni 600.

Ameongeza kuwa mradi utakapokamilika mwezi Mei 2021 Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 840 kati yao  240 ni wa kozi za muda mrefu na 600 wa kozi za muda mfupi kati ya miezi mitatu na sita.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe (hawapo pichani) Mkoani Tanga baada ya kuweka jiwe la Msingi katika Chuo cha VETA na kutembelea  miradi kadhaa ya Serikali
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na   Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Pancras Bujulu akitoa ufafanuzi kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa VETA Korogwe mkoani Tanga.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la Msingi katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Korogwe kilichopo Mkoani Tanga. Kushoto ni Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Baadhi ya wakazi wa Halmashauri wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani)alipokuwa akizungumza nao  Machi 15, 2021.
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, (hawapo pichani) mkoani Tanga.

 





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad