Na Debora Sanja, Bunge
Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kupitia Wizara ya
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuweka msukumo wa kudai madeni
ambayo Shirika la Mawasiliano (TTCL) na Shirika la Posta linawadai
wateja wake.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Moshi Kakoso
wakati Kamati ilipotembelea ofisi za TTCL Jijini Dar es Salaam.
Alisema madeni yote sugu yakianza kulipwa yatasaidia mashirika hayo
kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kujiendesha kibiashara.
"Haya madeni ambayo TTCL na Shirika la Posta wanawadai wateja wao
yakianza kulipwa yataleta manufaa makubwa kwa mashirika haya kwa kuwa
yataweza kujiendesha kibiashara," alisema.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kulisaidia Shirika la Posta kwa
kulipunguzia changamoto mbalimbali ikiwemo kuwaondolea baadhi ya madeni
ili liweze kujiendeleza.
Aliitaka pia Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia magari Shirika hilo la Posta ili liweze kusimama vizuri.
Mheshimiwa Kakoso pia alimpongeza Waziri wa Mawasiliano na Teknojia ya
Habari Mheshimiwa Faustine Ndugulile kwa kazi nzuri aliyoifanya ya
kusimamia sekta ya mawasiliano ndani ya kipindi kifupi.
"Natoa pongezi sana kwa kazi nzuri, endelea kuzisimamia taasisi zako vizuri na kazi yako itaonekana, " alisema.
Alisema Kamati ipo tayari kushirikiana na Wizara yake na kwamba kama
kuna kikwazo chochote kinachohitaji mabadiliko ya sheria wasisite
kupeleka mapendekezo Bungeni.
Kwa upande wake Mheshimiwa Ndugulile aliishukuru Kamati kwa ziara hiyo
na kuahidi kushirikiana kwa karibu ikiwemo kuyafanyia kazi maelekezo
yote ambayo Kamati imeyatoa.
Kamati ya Miundombini mbali na kutembelea Ofisi za TTCL na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupokea taarifa za utekelezaji wa
majukumu yao pia ilipokea taarifa ya Shirika la Posta na Mfuko wa
Mawasiliano kwa wote (UCSAF)
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano (TTCL)Ndugu Waziri Kindamba akiwalezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu jinsi ambavyo Mkongo wa Taifa unavyofanya kazi wakati wajumbe hao walipotembelea katika Ofisi za TTCL Jijini Dar es Salaam, , kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Anne Kilango, Menyekiti wa Kamati Mheshimiwa Moshi Kakoso na kushoto ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile.
Meneja Biashara wa Shirika la Mawasiliano (TTCL) Ndugu Laibu Leonard akiwalezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu teknolojia ya simu zilizokuwa zinatumika zamani kwa ajili ya mawasiliano, wajumbe hao walitembelea Ofisi za Shirika hilo Jijini Dar es Salaam. Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakipewa maelezo ya jinsi gari la kufuatilia masafa ya redio linavyofanya kazi wakati walipotembelea katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakipewa maelezo ya jinsi gari
la kufuatilia masafa ya redio linavyofanya kazi wakati walipotembelea
katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es
Salaam, wa kwanza kushoto ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari Dkt. Faustine Ndugulile.
No comments:
Post a Comment