Mbunge wa Mtama – Nape Nauye (Katikati), Meneja wa NMB Lindi Shaban Kassali (Kushoto) na Dkt Dismas Masulubu,Mganga Mkuu Mtama (Kulia) wakimsukuma Mkuu wa wilaya ya Lindi – Shaibu Ndemanga kwenye kiti cha wagonjwa ambacho kilitolewa na benki ya NMB kwaajili ya Kituo cha Afya Mtama na Pangaboi za wilayani Mtama Mkoani Lindi muda mfupi baada ya NMB kukabidhi msaada wa Vifaa tiba kwa ajili ya Kituo cha Afya Pangaboi pamoja na Zahanati ya Mtama Katika Halmashauri ya Mtama wilayani Lindi vyenye thamani ya sh. Milioni 10.
Mkuu wa wilaya ya Lindi,Shaibu Ndemanga (Kulia) akipokea msaada wa Vifaa tiba kutoka kwa Meneja wa NMB Lindi – Sahaban Kassali (pili kushoto) kwa ajili ya Kituo cha Afya Pangaboi pamoja na Zahanati ya Mtama Katika Halmashauri ya Mtama wilayani Lindi vyenye thamani ya sh. Milioni 10 vilivyotolewa na Benki ya NMB. Wengine kutoka kulia ni Samuel Warioba,Mkurugenzi halmashauri ya Mtama,Nape Nnauye,Mbunge Mtama,Dkt Dismas Masulubu, Mganga Mkuu Mtama. Makabidhiano hayo yamefanyika jana katika kata ya Nachunyu kituo cha Afya Pangaboi na Mtama Zahanati.
**************************************
Benki ya NMB mkoani Lindi imetoa misaada ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 10 kusaidia kuboresha huduma za afya katika vituo vya afya Pangaboi na Mtama vya mkoani Lindi.
Vifaa hivyo ni vitanda vya kujifungulia 4, vitanda vya wagonjwa 2, viti vya magurugumu kwaajili ya wagonjwa 2, mashuka 20 na magodoro vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 10.
Vifaa tiba hivyo vilikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga huku Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye akishuhudia na kusema kuwa msaada huo ni kielelezo kuwa NMB ni rafiki wa karibu katika kusaidia afya na elimu wilayani humo.
“Nimekuwa nikitembea maeneo mengi wilayani hapa kupokea msaada mbalimbali ya NMB katika sekta ya afya na elimu na katika hili naomba niwashukuru sana” alisema Shaibu.Alisema msaada huo kwa zahanati si kitu kidogo na kwamba watauenzi kwa kutunza vifaa hivyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza katika haflka hiyo, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alishukuru Benki ya NMB kwa kuwa ya kwanza kupeleka tawi katika halmashauri hiyo na pia kutoa msaada kwa kituo hicho cha afya.Hata hivyo aliwataka wadau wengine kuendelea kusaidia kuimarisha sekta ya afya na elimu katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kukuza uchumi.
Aidha alisema kwamba wamefanikiwa kupata Sh milioni 50 kwa ajili ya kujenga zahanati ya Mumbu na kwamba serikali itawasilisha Sh milioni 500 za kujenga kituo cha afya.
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mtama, Wahida Omary alisema anashukuru NMB kwa kuwasaidia vitanda vya kujifungulia vitakavyosaidia wazazi. Alisema zahanati hiyo inazalisha wanawake 300 kwa mwaka na kuwepo kwa kitanda kingine ni msaada mkubwa kwao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Meneja wa NMB Lindi, Shaaban Kassari alisema wametoa vifaa tiba ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa kukabili changamoto za jamii ili kuwepo na ukuaji mzuri wa kiuchumi kwa kusaidia sekta za afya na elimu.
“ Kupitia wananchi hawa, ndipo biashara yetu inapofanikiwa na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi hii kupitia nyanja mbalimbali za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja,
changamoto za sekta ya afya kwa NMB ni jambo la kipaumbele, kwa kuwa afya ndio msingi wa uchumi na uzalishaji mali na ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya wananchi” alisema.
No comments:
Post a Comment