OLE LEKAITA AKEMEA VURUGU KITETO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 1, 2021

OLE LEKAITA AKEMEA VURUGU KITETO

Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita akivishwa vazi la asili la wafugaji kwenye harambee ya ujenzi wa shule ya awali Orpirkata kijiji cha Namelock, zilipatikana zaidi ya sh. milioni 8.
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita akizungumza juu ya amani kwa wakulima na wafugaji kwenye harambee ya ujenzi wa shule ya awali Orpirkata kijiji cha Namelock, zilizopatikana zaidi ya sh. milioni 8.

Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Edward Ole Lekaita, amekemea vikali watu wanaoendeleza mauaji kwa kuwaua wananchi mwenzao badala ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria endapo wakibaini wamefanyiwa makosa.

Ole Lekaita ameyasema hayo wakati akizungumza alipoongoza harambee ya ujenzi wa shule ya awali Orpirkata iliyopo kwenye kijiji cha Namelock, ambapo zaidi ya shilingi milioni 8 zilipatikana.

Amesema ni makosa makubwa kujichukulia sheria mkononi na kufanya mauaji kwani hakuna binadamu anastahili adhabu ya kifo hata kama amefanya makosa.

Amesema hivi karibuni kuna mkazi wa kijiji cha Amei aliuawa kutokana na mgogoro wa ardhi hivyo tukio hilo lisijitokeze tena ila kuwe na mazungumzo pindi kukitokea kutokuelewana.

"Nitashindwa kufanikisha maendeleo endapo vurugu na mauaji yakijirudia tena Kiteto kama awali, kwani badala ya kupambana na maendeleo nitakuwa nataroka Bungeni na kuja nyumbani kusuluhisha machafuko." Amesema Ole Lekaita.

Amesema vurugu za wafugaji na wakulima zinapaswa kufika tamati kwani kila mmoja ana haki hivyo jamii hizo mbili kubwa ziwe na utaratibu wa kutii matakwa ya matumizi bora ya ardhi katika shughuli zao.

Amesema viongozi wa CCM na serikali wanapaswa kusimamia haki ili kuwe na amani na mshikamano baina ya jamii hizo mbili kubwa wilayani Kiteto za wafugaji na wakulima.

"Pia nawaomba wazee wa kimila na viongozi wa madhehebu ya dini, kuhubiri amani na mshikamano ili wafugaji na wakulima waishi bila vurugu." Amesema Ole Lekaita.

Amesema kilimo ni muhimu na mifugo ni muhimu hivyo maeneo ya mifugo yaheshimiwe na mashamba yaheshimiwe kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.

"Kiteto itakuwa ya amani na tulivu endapo kila mmoja atamuheshimu mwenzake na kutambua kuwa wafugaji na wakulima wote tunategemeana." amesema Ole Lekaita.

Hata hivyo, mkazi wa kata ya Namelock, Isack Paresoi amesema baadhi ya wanasiasa huwa wanachochea vurugu kwa kushawishi wakulima wakapande mazao kwenye malisho ya mifugo ili baadaye wapate kura.

"Serikali inapaswa kuwachukulia hatua wanasiasa uchwara kama hao ambao wanasababisha vurugu kwa kuwachochea wakulima na wafugaji ili baadaye wachaguliwe." Amesema Paresoi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad