CORONA HAIJAATHIRI UPATIKANAJI WA MAFUTA-WAZIRI KALEMANI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 8, 2021

CORONA HAIJAATHIRI UPATIKANAJI WA MAFUTA-WAZIRI KALEMANI

 

 

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto), Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon (katikati) na Mhandisi Mkuu wa Vituo vya Upokeaji wa Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Yona Malago( kulia)wakikagua eneo la kupakulia mafuta bandarini wakati wa ziara ya waziri huyo ya kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, iliyofanyika Februari 07, 2021.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati) na Kaimu Katibu Mkuu, Mhandisi Leonard Masanja(kulia) wakipata maelezo ya namna mafuta yanavyopimwa kutoka katika meli hadi kuwafikia walaji kupitia mita za kupimia mafuta(Flow Meter), wakati wa ziara ya waziri huyo ya kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, iliyofanyika Februari 07, 2021.

Muonekano ya Sehemu ya mita za kupimia mafuta (Flow Meter) kutoka katika meli hadi katika mataki ya kuhifadhia mafuta, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, ya kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, iliyofanyika Februari 07, 2021.

Mpira mweusi ukipakuwa mafuta Melini nakupita katika mita za kupimia mafuta (Flow Meter) hadi katika mataki ya kuhifadhia mafuta, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ya kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, iliyofanyika Februari 07, 2021.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto), Kaimu Mkuregenzi Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon (kulia) wakiwa katika chumba maalum (Contolroom) kufuatilia upimaji wa mafuta yanayoingia nchini kutoka melini kwa kutumia teknolojia ya kisasa wakati wa ziara ya waziri huyo ya kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, iliyofanyika Februari 07, 2021.

……………………………………………………………………………..

Zuena Msuya Dar es Salaam, 

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewatoa hofu watanzania kwa kusema kuwa tishio la virusi vya ugonjwa wa corona halijaathiri upatikanaji wa mafuta nchini.

Aidha kuna ziada ya mafuta itakayotumika zaidi ya siku 30 na bado meli zinaendeleapakuwa mafuta bandarini.

Dkt. Kalemani alisema hayo Jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya kutembelea bandari ili kujiridhirisha kama kuna mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji yanayohitajika nchini, kwakuwa nchi imeingia Uchumi wa Kati na miradi mingi mikubwa inaendelea kutekelezwa.

Alisema Tanzania imejipanga vizuri katika suala la upatikanaji wa mafuta, pia aliwatoa hofu watanzania kuwa serikali inaendelea vizuri katika sekta hiyo kwani mpaka sasa, hakuna kiwango cha mafuta kilichopungua tangu kutangazwa kwa uwepo wa ugonjwa huo duniani kote.

Alisema kwa sasa, nchi ina mafuta mengi na ya kutosha, pia ziada ya lita Milioni 209 kwa mafuta Petroli, mafuta ya Diseli lita Milioni 121, Mafuta ya Taa lita laki 6, na Mafuta Ndege lita Milioni 18, ambayo yatatosha kutumika kwa zaidi ya siku 30 zijazo na bado meli zinaendelea kupakuwa mafuta bandarini: Leo kuna meli inapakua Tani 38 za Mafuta.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuna  mafuta ya kutosha siku zote ili miradi mikubwa ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa kama vile ya SGR, Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, Miundombinu ya Barabara, Maji na mingine mingi isikwame kwa kukosa mafuta kutokana na ugonjwa huo.

“Ninawahakikishia watanzania kwa niaba ya serikali kuwa mafuta yapo na yataendelea kuwepo, tumshukuru Rais wetu, Dkt. John Magufuli  kwa msimamo wake thabiti kwani anatuwezesha kufanya kazi usiku na mchana, hivyo hatutaweza kuathirika kwa yanayosemwa, tumekaa na wadau pamoja na wataalamu wetu tumeweka mpango na mikakati ya kuhakikisha mafuta yanapatikana muda wote”, alisema Dkt. Kalemani.

Kuhusu matumizi ya mafuta nchini, Dkt. Kalemani alisema kuwa matumizi yanaongezeka siku hadi siku, ambapo kwa sasa tunatumia Mafuta lita Milioni 5.7 ya Diseli, Petroli lita Milioni 4.6, Taa lita zaidi ya laki moja, na Ndege lita zaidi ya laki 6.

Aidha alisema kuwa, matumizi ya mafuta ya Taa yamepungua kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa katika shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii vijijini.

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa, Mwaka jana nchi ilikuwa na jumla ya mafuta ya ziada ya lita Milioni 325, mwaka huu kuna ziada ya lita Milioni 412, hivyo amewataka wataalamu wanaosimamia sekta hiyo kuhakikisha kiwango cha upatikanaji wa mafuta kinaongezeka zaidi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa bandari, lazima kuendelea kupima na kuongeza uwezo wa bandari hizo nchini, ambapo kwa sasa imeongezeka bandari ya Tanga na Mtwara.

“Mpango mathubuti wa serikali ni kuangalia uwezekano wa kuongeza bandari kavu au maghala ya kuhifadhi mafuta katika Mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera zitakazotumika kuhifadhi mafuta ya takayosafirishwa nje ya nchi”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Katika hatua nyingine, aliwataka wawekezaji kuja kufanya utafiti na kuwekeza katika sekta ya mafuta, kwa kuwa bei ya mafuta katika soko la Duniani inaendelea kuongezeka ikilinganishwa  na miaka ya nyuma, na kueleza kuwa mwaka jana Pipa la mafuta ghafi lilikuwa Dola 50, ambapo kwa sasa ni Dola 57, Mafuta safi ilikuwa Dola 278, na sasa ni wastani wa Dola 446.

Katika ziara hiyo alitoa onyo kwa baadhi ya watanzania kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ya mafuta, ikitokea mtu amekamatwa kwa kosa hilo ahukumiwe kama wahujumu uchumi wengine kulingana na sheria za nchi: Pia Wataalamu pamoja na Timu ya Ulinzi na Usalama kuendelea kulinda na kusimamia miundombinu hiyo kwa maslahi mapana ya nchi na watanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad