Baraza la Madiwani Busega lapitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 16, 2021

Baraza la Madiwani Busega lapitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

 baraza la bajeti.jpg

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega limepitisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, katika kikao cha baraza kilichofanyika tarehe 15 Februari 2021 katika ukumbi wa Silsos.


Baraza hilo limepitisha Rasimu ya Bajeti yenye makisio yenye thamani ya TZS 35,175,907,278, ambapo fedha kutoka Serikali kuu ni tzs 30,297,052,209 amabayo ni asimilia 86.2, fedha za wahisani ni 2,814,855,069 sawa na asilimia 8 na fedha za mapato ya ndani TZS 2,064,000,000 amabyo ni asilimia 5.9. Kwa upande mwingine madiwani wamepongeza uandaji wa Baheti ya mwaka huu na kukiri kwamba ina mabadiliko makubwa ukilinganisha na Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambayo ilikuwa TZS 28,352,434,811.


Awali Mwenyeki wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe ameeleza kwamba utekelezaji wa Bajeti hiyo kunategemea sana kwa upatikanaji wa mapato hasa mapato ya ndani, hivyo ni lazima kutilia mkazo makusanyo ya mapato ya ndani. “Naomba suala la ukusanyaji wa mapato liwe kipaumbele na kutiliwa mkazo, Busega sio masikini, tunahitaji usimamizi bora kwenye suala hili, kwani mapato ya ndani ndio uhai wa halmashauri yetu.” aliongeza Mhe. Muniwe.


Aidha, hoja za baadhi ya madiani zilijitokeza, miongoni mwa hoja hizo ni kutaka kujua ni lini stendi ya Wilaya inayoendelea kujengwa itaanza kufanya kazi. Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema stendi ya Wilaya iliyopo makao makuu ya Wilaya, ipo kwenye hatua nzuri kwani kwasasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa Kalvati mbili kwaajili ya njia ya kuingia na kutoka na itakapokamilika muda wowote itaanza kutumika, na kuongeza kwamba kuanza kwa matumizi ya stendi hiyo kunategemea ushauri kutoka kwa wataalam kuhusu ni muda gani matumizi rasmi yaanze baada ya kumalizika kwa ujenzi wa Kalvati.


Kwa upande mwingine, diwani wa kata ya Nyashimo Mhe. Mickness Mahela alitaka kujua ni lini kituo cha afya Nassa kitapata Jokofu la Kuhifadhia Maiti. Akitoa maelezo ya jambo hilo Afisa Mipango wa halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Juma Rahisi amesema suala la ununuzi wa Jokufu kwaajili ya kituo cha afya Nassa lipo kwenye bajeti inayoendelea na utekelezaji wake lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa pesa lakini mpango wa ununuzi wa Jokofu kwaajili ya kituo hicho upo kwenye mpango na pesa zitakapopatikana za kutosha Jokofu litanunuliwa.

 

Vipaumbele 17 Vimeanishwa katika Rasimu hiyo ya Bajeti kupitia Mapato ya Ndani:

·         Kuchangia miradi ya maendeleo kwa shughuli zinazoanzishwa na wananchi kama njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi zao.

·         Kulipa posho za vikao na stahiki za Waheshimiwa Madiwani za kila mwezi.

·         Ujenzi wa miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari.

·         Kuendeleza shughuli mbalimbali za Ardhi wilayani.

·         Kugharamia zoezi la usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vya ndani na kukusanya takwimu kwa kila chanzo.

·         Kugharamia ujenzi wa masoko ya Masanza, Mwamagigisi, na Nyashimo.

·         Kuendeleza ujenzi wa stendi ya Nyashimo.

·         Kuboreha huduma za uvuvi.

·         Kuhamasisha ufugaji bora na kutoa chanjo za mifugo.

·         Kuongeza vitendea kazi kama vile pikipiki na magari.

·         Kuboresha huduma za Afya.

·         Kugharamia uendeshaji wa Ofisi na vikao mbalimbali vya kisheria.

·         Kujenga vizimba vya kufugia Samaki ili kujiongezea mapato.

·         Kuendeleza shughuli za ugani kama kilimo cha mazao ya biashara na chakula na mifugo kwa kuhamasisha wananchi kupanda mbegu bora za Pamba na kuanzisha mashamba darasa ya mazao ya Pamba na Alizeti.

·         Kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali, Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

·         Kuboresha usafi wa mazingira.

·         Kugharamia malipo ya vibarua.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad