MUZIKI WETU SHOWCASE YALENGA KUWAINUA WASANII NCHINI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, January 30, 2021

MUZIKI WETU SHOWCASE YALENGA KUWAINUA WASANII NCHINI

 

Mkuu wa Idara ya ushirikiano na utamaduni kutoka ubalozi wa Ufaransa nchini Cecile Frobet (katikati,) akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusiana na mfululizo wa matamasha mubashara kwa wasanii chipukizi ikiwa sehemu ya kuonesha na kupata fursa za kuutangaza utamaduni wa Tanzania nje ya nchi, kushoto ni mratibu mradi kutoka shirika la ASEVADA Tanzania.


Msanii na muongozaji sanaa Isack Abeneko akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mfululizo wa matamasha hayo yatakayofanyika mubashara katika ukumbi wa wazi wa kituo cha utamaduni cha ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya wadau na waandishi wa habari wakifuatilia mjadala huo, Leo jijini Dar es Salaam.


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

UBALOZI Wa Ufaransa nchini kupitia kituo chake cha utamaduni cha Alliance Francaise na shirika la ASAVEDA Tanzania wameandaa Tamasha maalumu la burudani la "Muziki wetu ShowCase," lenye lengo la kuwainua wasanii chipukizi na kutoa fursa kwa wasanii wakubwa kutangaza utamaduni wa Tanzania kupitia Muziki nje ya Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam  Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Utamaduni kutoka ubalozi wa Ufaransa nchini Cecile Frobet  amesema kuwa Serikali ya Ufaransa kupitia ubalozi wake nchini Tanzania utaendelea kushiriki katika kueneza utamaduni wa Tanzania na hiyo ni kwa kuwaunganisha wasanii kutoka mataifa hayo mawili na kushirikishana tamaduni za nchi hizo mbili.

Amesema, Tamasha hilo litafanyika kwa mfulilizo ndani ya miezi sita kwa kuwa na tamasha moja kila mwezi, na Tamasha la kwanza litaanza Februari 4 mwaka huu na mapato yatakayopatikana yataelekezwa kuwasaidia wasanii chipukizi katika kutafuta fursa.

Amesema kuwa, Jukwaa hilo lipo wazi kwa wasanii chipukizi kuonesha vipaji vyao pamoja na kukutana na wasanii wakubwa na kubadilishana uzoefu wa kazi.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi kutoka Shirika la ASEVADA Tanzania Joy Sendama amesema,shirika hilo linafanya kazi bila faida na limekuwa likisimamia miradi mbalimbali yenye kuleta tija kwa jamii ikiwemo Muziki.

Joy amesema, kupitia Muziki wetu ShowCase wasanii chipukizi watapata  fursa ya kutangaza vipaji vyao na kuweza kutambulika zaidi.

Vilevile msanii na muongozaji wa wasanii Isack Abeneko amesema kuwa Tamasha limeratibiwa na ASEVADA kwa kushirikiana na BASATA na Alliance Francaise kupitia ubalozi wa Ufaransa nchini litatanguliwa na Tamasha la Sauti za Busara 2021 ambapo baadhi ya wasanii wa Muziki wetu ShowCase watatumbuiza kwenye jukwaa hilo kubwa barani Afrika.

Amesema, jukwaa la Muziki wetu ShowCase linaonesha aina mbalimbali za Muziki mubashara ukiwemo Bongo Fleva, Singeli, taarabu na mduara.

Kuhusiana na gharama za viingilio ambavyo vimeelekezwa kuwainua wasanii chipukizi Isack amesema, kiingilio kwa wanafunzi ni sh. elfu tano tuu na wakubwa ni sh.elfu kumi tuu na litaanza saa mbili usiku  kuanzia tamasha la kwanza la Februari 4 katika ukumbi wa wazi wa Alliance Francaise huku wakitegemea kuwakusanya wana vyuo wengi zaidi kwa kuwa ndio hadhira kubwa ya Taifa katika kueneza utamaduni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad