HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 3, 2020

‘TAWLA’ YAMPONGEZA JAJI MKUU KWA TUZO

 Na Mary Gwera, Mahakama

Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimempatia tuzo ya pongezi Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufuatia jitihada zake za kuhakikisha wanawake na watoto wenye uhitaji maalum  wanapata haki.

Akikabidhi tuzo hiyo maalum kwa Mhe. Jaji Mkuu mapema jana Desemba 02, 2020 ofisini kwa Mhe. Jaji Mkuu, Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ‘TAWLA’, Bi. Lulu Ng’anakilala alisema kuwa Chama hicho kinatambua na kupongeza jitihada za Mhe. Jaji Prof. Juma kwa kuhakikisha kuwa haki za akina mama na watoto zinapatikana na kumpongeza kwa jitihada za kuhakikisha mashauri ya mirathi yanaondoshwa kwa wakati.

“Tunashukuru kwa kuendelea kutuunga mkono katika kuhakikisha kuwa haki za wanawake na watoto zinapewa umuhimu wake, katika hili tunatambua jitihada zako za dhati na hivyo tumeona ni vyema tukukabidhi tuzo hii maalum ili kutambua mchango wako,” Bi. Ng’anakilala alimueleza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Mhe. Jaji Mkuu alishukuru kwa tuzo hiyo na kuwahakikishia wanachama wa Chama hicho kuwa ataendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka wanachama hao kushiriki na Mahakama katika kuelezea wananchi kuhusu taarifa mbalimbali za Mahakama ikiwemo maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji haki inapatikana kwa wakati.

Mhe. Jaji Prof. Juma alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanapata taarifa sahihi za Mahakama kwa kutembelea vyanzo vya habari vya kiofisi ikiwemo Tovuti ya Mahakama ambayo ni www.judiciary.go.tz.

“Ili kupata taarifa sahihi za Mahakama endapo taarifa husika haipo kwenye gazeti au chombo kingine cha habari ni vyema kutembelea vyanzo rasmi vya habari zetu ikiwemo tovuti ya Mahakama ambapo kupitia vyanzo hivyo mtu anaweza taarifa muhimu ikiwemo kujua kesi yake imefikia wapi na kadhalika,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TWALA), Bi. Lulu Ng’anakilala. Tuzo hiyo amepatiwa na Chama hicho kwa kutambua mchango mkubwa wa kuhakikisha wanawake na watoto wenye uhitaji maalum wanapata haki. 


Mazungumzo yakiendelea kati ya Mhe. Jaji Mkuu na Wageni kutoka TAWLA, mazungumzo hayo yalifanyika kabla ya kukabidhi tuzo. (Picha na Mary Gwera, Mahakama)



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad