HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 15, 2020

WOFATA KUWASAIDIA WANAWAKE KUJIKWAMUA KIUCHUMI

 

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utetezi wa haki ya Afya kwa wasichana na wanawake Tanzania (WOFATA) limesaidia kuwakwamua wanawake na wasichana wa mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Singida kutokana na changamoto ya kiuchumi wakati wa ugonjwa wa Covid-19.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Shirika la WOFATA, Mpendwa Chihimba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu kumalizika kwa mradi wa kuwawezesha wanawake kutoyumba kiutu na kiafya kipindi cha Covid-19, uliotekelezwa na shirika lake.

Chihimba alisema “WOFATA kupitia ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT), kwa kipindi cha miezi mitatu ya katikati ya Julai 2020 hadi katikati ya Oktoba 2020, limefanya shughuli za kusaidia baadhi ya wanawake katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Singida ikiwa ni sehemu ya mapambano ya kujikinga na virusi vya Corona ili kuzuia kupata ugonjwa wa COVID -19”. Katika mapambano hayo, shirika lilihakikisha linapunguza athari zilizosababishwa na virusi hivyo nchini na makovu yaliyochangiwa na uwepo wa virusi hivyo na ugonjwa wa Covid-19 pamoja na kudidimia kwa vipato vya wanawake na makundi mengine katika jamii, aliongeza. Alisema kuwa katika kipindi cha mwanzo virusi vya Corona vilipoingia nchini, wanawake wanawake wengi wakiwemo wajasiliamali katika masoko na sehemu za mikusanyiko walishindwa kutekeleza majukumu yao kwa hofu ya virusi hivyo.

Kuhusu wanawake wenye mahitaji ya kiafya Mkurugenzi Chihimba alisema kuwa walishidwa kufukia huduma za matibabu. “Wanawake na wasichana wenye mahitaji ya kiafya ikiwemo wajawazito na wenye uhitaji wa huduma za mara kwa mara hospitalini walishindwa kufikia huduma hizo kutokana na sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni woga wa kwenda kufuata huduma za afya na matibabu katika zahanati, vituo vya Afya na hospitali. Kufuatia changamoto hizo, WOFATA waliweza kujipanga ili kusaidia kuwakwamua wanawake na wasichana ambao ni wanachama wa WOFATA na wengine wanaowazunguka katika baadhi ya maeneo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Singida” alisema Chihimba.

Kwa upande wake, Minza Joram alisema kuwa vitendo vya unyanyasaji kijinsia vilikuwepo japokuwa ni vigumu kuonekana. Alisema kuwa kufuatia mfumo dume katika maeneo mengi, wapo wanawake waliopoteza mitaji yao ya biashara kwa mitaji hiyo kuchukuliwa na wenza wao. “Mambo kama haya unakuta ni ukatili kwa wanawake lakini kwa sababu hayasemwi hivyo, hayafahamiki katika jamii. Nenda mfano kwenye taasisi za kifedha, utakuta malalamiko ya baadhi ya kina mama kushindwa kulipa mikopo yao ni kutokana na wenza wao kuchukua mitaji kinyume na malengo” alisema Joram.

Shirika la WOFATA lenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam lilianzishwa mwaka 2002, likiwa na matawi katika mikoa 17 ya Tanzania bara.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad