HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 15, 2020

Jamii yapewa wito kujenga utamaduni wa kufanya vipimo vya hali ya lishe

 



NJOMBE

Jamii mkoani Njombe na Tanzania kwa ujumla wametakiwa kuwa na utamaduni wa kufanya vipimo vya hali ya lishe angalau mara mbili au tatu kwa mwaka ili kufahamu hali yake ya lishe na kumsaidia kufuata njia bora za lishe ili kuepuka utapiamlo.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mtafiti Mwandamizi-Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bi.Maria Ngilisho kwenye mwendelezo wa maonesho ya Wiki ya Chakula Duniani iliyozinduliwa rasmi tarehe 10/10/2020 ambapo  Kitaifa maadhimisho haya yanafanyika Mkoani Njombe na yatahitimishwa 16/10/2020.

Bi.Ngilisho amesema, moja ya vipimo vinavyoweza kutoa tafsiri ya kuwa na hali nzuri ya lishe ni kipimo cha uwiano kati uzito na kimo/urefu ili kupata farihisi (Body Mass Index - BMI).

Amesema, kabla ya kufanya vipimo vya hali ya lishe katika banda lao, mteja anaeleweshwa namna ya kupanda kwenye mizani  (kuvua viatu, kutoa vitu mfukoni kama vile funguo, simu na vitu vingine ambayo vinaweza kuongeza uzito wake kama vile saa) na kusimama kwenye ubao wa kupimia kimo/urefu (kuvua viatu; mgongo kuwa sambamba na ubao; makalio, mabega na kisogo viguse ubao; kusimama wima na kuangalia mbele)", alisema Bi. Ngilisho.

Aliendelea kwa kusema, baada ya vipimo kuchukuliwa, vinaoanishwa kwa kutumia kadi ya farihisi ili kupata tafsiri ya hali yake ya lishe na kupewa ushauri stahiki kufuatana na matokeo ya vipimo vyake.

Aidha Bi. Ngilisho alisema, katika kurahisisha uelimishaji wa njia sahihi ya kupanga mlo kamili kwa jamii ni kutumia dhana ya pitamidi ya chakula (muundo wa kabati iliyotenganishwa katika vyumba vitano, chumba kikubwa kikiwa chini na kidogo kabisa kikiwa juu). Kila chumba katika piramidi hii kina wakilisha kundi moja la chakula, ili kupata/ kuandaa mlo kamilo inatakiwa kuchukua angalau chakula kimoja kutoka kwenye kila kundi/chumba.

"Kundi la kwanza lina  vyakula vya nafaka (mahindi, ngano, ulezi, mtama, uwele, nk.),  mizizi (mihigo, viazi vitamu, viazi mvitingo, magimbi, nk.) na ndizi (ndizi mbichi).Kundi la pili lina vyakula vya asili ya wanyama (nyama ya ng'ombe, kuku, mbuzi, nk., maziwa, mayai, dagaa, samaki na wadudu waliwao kama senene na kumbikumbi. Jamii ya mikunde ni kama maharage, njegere, mbaazi, kunde, choroko, soya, nk.). 

Kundi la tatu ni la mboga za majani (mchicha, spinachi, chinise, figiri, tembele, nk.) na mboga-mboga (pilipili hoho, karoti, vitunguu, nyanya, bamia, biringanya, nyanya chungu, matango, nk.), bila kusahau mboga za asili na porini. Kundi la nne ni la matunda ya aina mbalimbali kama machungwa, maembe, mananasi, ndizi mbivu, limao, fenesi, parachichi, machenza, nk., ukijumuisha pia matunda ya asili na matunda ya porini. Kundi la tano la tano linajumuisha vyakula kama sukari, mafuta, karanga, ufuta, korosho, mbegu mbalimbali kama vile mbegu za alizeti, maboga na nazi" Alisema Bi.Ngilisho.

Nae afisa lishe mtafiti kutoka taasisi hiyo, Elizabeth Lyimo, alielezea kuhusu mchezo wa karata za mlo kamili ambao lengo lake ni kuboresha uelewa wa wananchi kuhusu mlo kamili kwa njia shirikishi na ya kufurahisha ili kuvutia washiriki kujifunza.

"Mtu yeyote anaweza kucheza mchezo wa karata za mlo kamili. Masuala ya chakula katika ngazi ya kaya yanatekelezwa kwa asilimia kubwa na wanawake, wanaume wamekuwa wakishiriki kwa kiwango kidogo hivyo basi mchezo huu unawalenga zaidi wanaume wa rika zote ili wapate uelewaa wa kupanga mlo iwe katika kununua vyakula au kuandaa mlo kwa ajili ya familia. " Alisema Elizabeth.

Aidha Mteknolojia Mwandamizi wa Maabara kutoka taasisi ya chakula na lishe Juvenary Mushumbusi alisema taasisi ina Maabara
mahususi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa
kimaabara ili kuiwezesha Taasisi kutekeleza na kufanikisha majukumu yake.

Maabara hii ina vitengo vitatu, ambayo ni;
• Mabara ya Kemia ya Chakula (Food Chemistry
 Laboratory)
 Kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa
 sampuli za chakula ili kubaini uwepo na wingi wa viinilishe
 kama vile, protini, wanga, mafuta, vitamini, madini na phytochemicals. Pia kitengo hiki hufanya uchunguzi wa kubaini ubora na usalama wa chakula Kama vile uwepo na wingi wa  sumukuvu, madini tembo, sumu kwenye
 mihogo (cyanide) na vikolezo (food additives)

• Maabara ya Baiokemia (Biochemistry
 Laboratory)
 Kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa  sampuli zinazochukuliwa kutoka kwenye mwili wa  binadamu ili kubaini viwango vya virutubishi au  viashiria lishe mwilini (Nutritional Biomarkers) mwilini; kwa mfano, vitamin, madini na elementi mbalimbali, mafuta na wingi wa damu
• Maabara ya Maikrobiolojia (Microbiology
 Laboratory)
 Kazi kubwa ya maabara hii ni kufanya vipimo maalumu vya kilishe Kama vile folate na amino asidi kwa kutumia mbinu za maikrobiolojia.

Pia maabara hii hupima vimelea vinavyo patikana kwenye chakula ili kubaini usalama na ubora wake kimikrobiolojia km vile uwepo wa vijidudu vinavyosabisha magonjwa kwa mtumiaji wa chakula au vile vinavyoashiria kuharibika kwa chakula au vinavyoashiria hali ya usa lama wa  maeneo/mazingira yanayuhusika na  utayarishaji/usindikaji wa chakula husika. Baadhi ya vimelea hivi ni kama Salmonella, E-coli,Shigella na S.aureus

Juvenali Msumbusi ni mtekinolojia mwandamizi wa maabara kutoka taasisi ya chakula na lishe taifa,amesema kulingana na maeneo ya nyanda za juu kusini mimea kukosa virutubishi,serikali imekuja na mpango wa kuongezea virutubishi kwenye chakula.

"Serikali saizi imekuja na mpango mwingine wa kuongezea virubishi kwenye vyakula kama unga wa mahindi na ngano na virutubishi hivi havibadilishi rangi wala radha na kwenye upande wa vitamini A tunaongeza virubishi kwenye mafuta ya kura"alisema Juvenali Msumbusi

Aidha amewata wananchi kufika na kupata elimu katika taasisi hiyo licha ya wao kutumia njia mbali mbali ili kumalizana na tatizo la udumavu ikiwemo kwa watoto wadogo.

Elizabeth Lyimo ni afisa lishe mtafiti kutoka taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) akiendelea kutoa mafunzo juu ya lishe kwa wananchi waliofika katika banda hilo kwenye maonesho mjini Njombe.
Juvenali Msumbusi mtekinolojia mwandamizi wa maabara kutoka taasisi ya chakula na lishe taifa akionesha namna ya ukaushaji wa mboga mboga na matunda bila kupoteza vitamini
:Mmoja wa wataalamu kutoka taasisi ya chakula na lishe taifa  akiendelea na zoezi la kuwapima wananchi waliofika katika banda hilo kwenye maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayofanyika kitaifa mjini Njombe.


 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad