HEDHI APP YA UTOAJI WA ELIMU YA AFYA KWA WANAWAKE YAZINDULIWA JIJINI DAR - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 22, 2020

HEDHI APP YA UTOAJI WA ELIMU YA AFYA KWA WANAWAKE YAZINDULIWA JIJINI DAR

Mkurugenzi Mkuu wa AnuFlo Industries Ltd, Flora Njelekela akiongea na wanahabari wakati wa uzinduzi wa Hedhi App  jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa AnuFlo Industries Ltd,  Flora Njelekela (Kushoto) akiongea na mwanahabari wakati wa uzinduzi wa Hedhi App jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na Meneja kutoka Selcom, Saumu Rajabu (kulia).
Mkurugenzi Mkuu wa AnuFlo Industries Ltd, Flora Njelekela (Kushoto) akisimama pamoja na Saumu Rajabu (kulia) Meneja kutoka Selcom.
Daktari Berno baada ya uzinduzi wa Hedhi App. Daktari Berno ndiye mmoja wa madaktari ambaye atakuwa anazugumza na wanawake kupitia Hedhi App.

Na Mwandishi Wetu.

Kiwanda cha AnuFlo Industries kimezindua app maalumu kwaajili ya kutoa elimu ya afya kwa wanawake kuhusu hedhi na afya ya Uzazi. App hiyo inatoa fursa kwa wanawake na mabinti kuzungumza moja kwa moja na madaktari bingwa au wataalamu wa magonjwa ya wanawake kwa njia ya faragha.

App ya Hedhi itawasaidia watumiaji kununua bidhaa kwaajili ya matumizi yao binafsi na kutunza afya zao kwaajili ya kujenga maisha bora. 

App hiyo ni ya bure na ya kwanza nchini kutumia lugha ya Kiswahili ambapo inalenga kuwasaidia watumiaji kufahamu mzunguko sahihi wa siku zao za hedhi, kufahamu masuala ya ujauzito, kutoa vidokezo na taarifa muhimu kutoka kwa wataalamu wa afya.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kiwanda cha AnuFlo Industries, Flora Njelekela, app hiyo inawasaidia wanawake kufahamu mabadiliko yoyote yatakayojitokeza katika mzunguko wa hedhi. Pia inamwezesha mtumiaji njia ya kufuatilia mabadiliko yanayohusu mihemko na mwili wake kwa ujumla. Aidha inasaidia kujifunza jinsi mzunguko wako wa hedhi unavyoathiri mwili wake.

“Hii ni nyenzo muhimu kwa mabinti kwaajili ya kufautilia mzunguko wao wa hedhi na pia kufuatilia hatua mbalimbali za mabadiliko katika mwili. Kwa mujibu wa tafiti zetu, tumegundua kwamba mabinti wengi wanapata mimba zisizotarajiwa kutokana na kukosa taarifa sahihi juu ya mzunguko wa hedhi. Ujio wa app hii ya Hedhi utawasaidia kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi na kudhibiti mimba zisizotarajiwa. Walengwa watapata fursa ya kuzungumza na madokta mabingwa wa wagonjwa ya wanawake kwa njia ya faragha. Tunaamini kuwa jitihada hizi zinawasaidia sana walengwa kumudu mzunguko wa hedhi na kupata elimu ya afya uhusiano wa jinsia kwa ujumla,” alisema Mkurugenzi huyo 

Aliongezea kusema kuwa “Kwa maana hiyo, kutokana na utafiti wetu, tunaongeza ufahamu na kutoa elimu kwa mabinti na wanawake, walimu, vijana wa kiume na akina baba juu ya suala zima la hedhi. Tuna mpango wa kutembelea shule za mbalimbali za vijijini na kuweka utaratibu maalumu wa mawasiliano kwa mabinti wasiokuwa na simu janja ili waulize maswali mbalimbali juu ya hedhi kwa kuwafikia madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama, walimu. Wakati huo huo tuna mpango wa kuwa na vitabu maalumu vitakavyowasaidia mabinti wa vijijini kufuatilia kwa usahihi mzunguko wao wa hedhi.” 

Kwa sasa nchini Tanzania, msichana mmoja kati ya wanne (23%) wa umri kati ya miaka 15 na 19 ama amezaa au ni mjamzito. Mimba za utotoni kwa Tanzania zimekuwa zikitokea sana katika maeneo ya vijijini. Ni asilimia 26, tofauti na mijini ambapo ni asilimia 15. Asilimia 91 ya maduka ya vijinini hayauzi bidhaa zinazohusiana na hedhi na hata kama zinapatikana bado kuna hali ya unyanyapaa na miiko mingine ya kiutamaduni pale muhusika anapokwenda kununua. Unyanyapaa katika jamii juu ya masuala ya hedhi ni kikwazo kwa mabinti na akina mama kufanya uamuzi sahihi wakati wa hedhi. Nchini Tanzania katika maeneo ya vijijini kuna vikwazo mbalimbali kwa wasichana walioko katika hedhi. Kwa mfano, kuzuiwa kuchota maji, kupika, kuosha vyombo, kugusa mimea fulani au kupita kwenye shamba lililolopandwa mazao. 

Tafiti zaidi zinaonesha kuwa, asilimia 48 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo wanapokuwa katika hedhi. Hii ina athari kubwa kutokana na ukosefu wa elimu.

Vijana wa kike pia ni waoga linapokuja suala la ununuzi wa bidhaa za usafi kwaajili ya usafi wao, ununuzi wa bidhaa za uzazi wa mpango au dawa zinazohusiana na mfumo wa uzazi

Hii inasababishwa na mazoea ambayo yamekuwepo katika maisha ya kila siku. App ya Hedhi itaondoa tofauti hizi na kutoa fursa kwa walengwa kuwa huru kuagiza bidhaa hizo husika ikiwamo dawa za uzazi wa mpango au kondom, na bidhaa nyingine husika kupitia app hii, kuhakikisha zinawafikia hadi mlangoni. Hii pia ilichangiwa na ukosefu wa elimu

Hii ndiyo sababu kubwa, kwanini Kiwanda cha AnuFlo Industries kilifikiria kuja na app ya Hedhi ambayo itawasaidia mabinti kutambua mzunguko sahihi wakati wa hedhi. Kiwanda cha AnuFlo kitatoa semina kwa wasichana kwa maeneo ya vijijini na mijini ili kuongeza ufahamu katika elimu ya afya kwa wanawake na pia kuwafundisha namna ya kutumia app ya kwa manufaa yao.

Kwa upande wake, Dokta Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Dr Living Colman, kutoka Hospitali ya Muhimbili alisema: “Tuna furahi kushirikiana na Kiwanda cha AnuFlo kupitia app hii ambapo uzoefu unaonesha kuwa, wanawake walio wengi wanaogopa kuonana na wataalamu wa magonjwa ya akina mama. Tunafurahia hatua hii ya kutoa ushauri kwa akina mama na kuwahakikishia kuwa taarifa inayotolewa ni siri kati ya mtoaji na mpokeaji. Tutakuwa tunajadili mada mbalimbali kuhusu mambo muhimu na hasa yanayohusu mzunguko wa hedhi na mfumo wa uzazi.”

App ya Hedhi imebuniwa katika mfumo maoni na mrejesho kutoka kwa watumiaji ambao wanahitaji kujifunza kwa urahisi kuhusu mzunguko wa wao wa hedhi.

Hii ni app ya kwanza nchini Tanzania ikiwa katika lugha ya Kiswahili ambayo pia inawahusisha madakatri bingwa wa magonjwa ya wanawake.

AnuFlo Industries wameungana na kampuni za Selcom and Vodacom ili kurahisisha mfumo wa malipo kupitia Selcom na pesa endapo mtuamiaji atahitaji kufanya malipo ya aina yoyote kwa huduma zaidi atakayohitaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad