Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto
James, akifunga Kongamano la Wanamipango la Mwaka 2020, ambapo ameahidi
Wanamipango (hawapo pichani) kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili wakati wa kutekeleza majukumu yao, jijini Dodoma.

Kamishna
wa Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Nicolaus Shombe,
akiahidi utekelezaji wa maadhimio waliyokubaliana kwa Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James,
ambaye ni Mlezi wa Wanamipango wote nchini (hayupo pichani), wakati wa
kufunga Kongamano la Wanamipango la Mwaka 2020, jijini Dodoma.

Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto
James, akiteta jambo na Kamishna wa Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha
na Mipango, Dkt. Nicolaus Shombe, wakati wa kufunga Kongamano la
Wanamipango la Mwaka 2020, jijini Dodoma.

Meza
Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji
Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James (katikati), kulia ni Kamishna wa
Mipango ya Kitaifa wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Nicolaus Shombe na
kushoto ni Kaimu Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Wiliam Mhoja, wakifuatilia maoni yaliyokuwa yakitolewa na Wanamipango
wakati wa Kongamano la Wanamipango la Mwaka 2020, jijini Dodoma.

Wanamipango
wakiendelea kufuatilia kwa karibu hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James, ambaye ni Mlezi
wa Wanamipango wote nchini wakati wa kufunga Kongamano la Wanamipango
la Mwaka 2020, jijini Dodoma.

Mkurugenzi
wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. John Cheo akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya Wanamipango wakati wa kufunga Kongamano la
Wanamipango la Mwaka 2020, jijini Dodoma.
(Picha na Josephine Majura , WFM – DODOMA).
**********************************
Na. Farida Ramadhani na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma
Wizara
ya Fedha na Mipango imeanza rasmi kuisimamia Kada ya Wanamipango nchini
ili kuwalinda na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kupanga na
kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini bila kuingiliwa.
Akizungumza
jijini Dodoma wakati wa kufunga Kongamano la Wanamipango la Mwaka 2020,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali,
Bw. Doto James alisema Wizara hiyo imewatambua rasmi Wanamipango kama
inavyofanya kwa Wahasibu, Wakaguzi na Wagavi.
“Tutawawezesha
kitaaluma maana nimesikia malalamiko mengi, nimeambiwa katika ngazi ya
Halmashauri Wanamipango nikama wametelekezwa, wanaitwa majina mengi
yanayowashushia morali ya kazi, kwa hiyo kuanzia sasa hatutokubali hilo
litokee kwa Wanamipango”, alisema.
Bw.
James alisema kuwa Wizara itatengeneza namna nzuri ya kuwasiliana na
Wanamipango wote nchini kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali
zinazowakabili na itawalinda kwa gharama yoyote wale wote wanaoonewa
katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Alisema
Wizara inaangalia namna ya kutenga Bajeti kwa ajili ya kuwawezesha
Wanamipango kutekeleza majukumu yao huku akiwatahadharisha kuwa fedha
hizo hizitatolewa kiholela kwa kuwa utatengenezwa utaratibu mzuri wa
kuwafikia wote ambao watafuata utaratibu wa matumizi ya fedha hizo
katika majukumu yao.
“Wanamipango
lazima ufuatilie kile ulichopanga na utekelezaji wake, kule kwenye
utekelezaji ndio kumekuwa na madudu, kitu chakufuatilia kila siku kwa
mwaka mtu haendi, wakija wakaguzi kwenye mradi na yeye ndio anaenda,
unakuta yeye ni mgeni kwenye mradi wake. Kila kitu hajui, mambo haya
hatutokubali yatokee tena”, aliongeza.
Bw.
James aliahidi kuyachukua masuala yote yaliyojitokeza kwenye
majadiliano na maazimio yaliyofikiwa katika kongamano hilo kwa kuwa
yatasaidia kufanikisha na kuboresha usimamizi wa upangaji na utekelezaji
wa sera na mipango ya maendeleo.
Naye
Kamishna wa Mipango ya Kitaifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.
Nicolaus Shombe, alisema katika kongamano hilo la siku mbili Wanamipango
walipata nafasi ya kujadili mada mbalimbali ikiwemo uandaaji wa Mpango
wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano unaotarajiwa kuanza mwaka 2021/22.
Alisema
walijadili kwa kina kada ya Wanamipango kuhusu umuhimu na mchango wake
katika maendeleo ya nchi na changamoto ambazo wanakumbana nazo katika
utendaji kazi zao pamoja na kutoa mapendekezo ya kukabiliana nazo.
Kwa
upande wa Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI,
Bw. John Cheo ambaye ni miongoni mwa washiriki wa Kongamano hilo
ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuchukua jukumu la kuwalea
Wanamipango kwa kuwa anaamini uamuzi huo utachochea ubunifu katika
kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo nchini.
No comments:
Post a Comment