Mkuu
wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele (kushoto),
akizungumza na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa
Umeme wa Rusumo kabla ya kuanza ziara ya kazi yenye lengo la kukagua
miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika,

Baadhi
ya wanafunzi wakiwa katika foleni kuingia chumba cha Daktari katika
Zahanati ya Kijiji cha Kyenda iliyoko wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera.
Taswira hii ilichukuliwa Septemba 28, 2020 wakati wa ziara ya Timu ya
Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
(pichani), kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi
huo. Zahanati hii imejengwa kupitia Mradi husika.

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
ikikagua tanki la maji linalojengwa katika Kitongoji cha Ngome, Kijiji
cha Kasulo, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera kupitia Mradi huo, Septemba
28, 2020. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya
kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
ikikagua nyumba ya kuishi walimu katika Shule ya Sekondari Mumiterama,
wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera iliyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo
ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa
na Mradi huo.

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
ikikagua ujenzi wa Tanki la Maji, eneo la Rusumo, wilayani Ngara, Mkoa
wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya
kijamii inayotekelezwa na Mradi huo .

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
ikikagua Jengo la Madarasa katika Shule ya Sekondari Mumiterama,
wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera iliyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo
ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa
na Mradi huo.

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
ikizungumza na wanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Rusumo
iliyoko kijiji cha Kyenda, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo
ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa
na Mradi huo Septemba 28, 2020 ambapo Shule hiyo imenufaika kwa
kujengewa vyumba vya madarasa na vyoo vya wanafunzi.

Sehemu
ya majengo ya Kituo cha Afya Rusumo, kilichoko wilayani Ngara, Mkoa wa
Kagera, kinachojengwa kupitia Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa
wilayani humo. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 28, 2020 wakati wa
ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo,
kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi
husika.

Baadhi
ya wajumbe wa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa
Umeme wa Rusumo wakijadiliana jambo nje ya Zahanati ya Kijiji cha
Kyenda, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera baada ya kufanya ukaguzi katika
Zahanati hiyo wakiwa katika ziara ya kazi, Septemba 28, 2020. Kutoka
kulia ni Kiongozi wa Msafara, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Kaimu
Kamishna kutoka Wizara ya Nishati na Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo,
Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa
Rubagumya kutoka TANESCO ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi.

Timu
ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo
wakijadiliana jambo baada ya kukagua vyoo vya wanafunzi katika Shule ya
Sekondari Mumiterama, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera vilivyojengwa
kupitia Mradi huo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi
mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.
…………………………………………………………………………..
Veronica Simba – Ngara
Serikali
imeeleza kuwa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji
ya Mto Kagera, unaotekelezwa Rusumo wilayani Ngara, una manufaa mtambuka
kwa Watanzania.
Hayo
yalielezwa jana, Septemba 28, 2020 na Timu ya Serikali kutoka Tanzania
inayosimamia Mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya
Ufundi, wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi
mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.
Akizungumza
baada ya ziara hiyo, Kiongozi wa Timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga
ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika, alisema mbali na umeme, Mradi
huo utawanufaisha Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii
ambayo alisema iko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Mhandisi
Luoga ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati
alieleza kuwa miradi ya kijamii inayotekelezwa ni pamoja na inayohusu
sekta za afya, elimu, maji, mifugo na kilimo.
Akizungumzia
lengo la Timu hiyo ya Serikali kutembelea miradi ya kijamii
inayoendelea kutekelezwa, Mhandisi Luoga alisema ni kujionea hatua
iliyofikiwa katika utekelezaji wake, kubaini changamoto zilizopo na
kuzitafutia ufumbuzi ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.
“Tumetembelea
shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya na miradi ya
maji ambayo yote inayotekelezwa hapa Ngara na tumejiridhisha kuwa kwa
sehemu kubwa imefkia hatua nzuri na baadhi yake imekamilika.”
Hata
hivyo, alieleza kuwa Timu yake imebaini changamoto ya baadhi ya miradi
kusuasua hususan Mradi wa Maji unaotekelezwa Rusumo ambao umechelewa
kutokana na kukosekana vibali vya ujenzi.
Alisema
yeyé na wenzake wametatua changamoto husika kwa kuelekeza vibali hivyo
vipatikane haraka ili Mkandarasi aanze kazi na kukamilisha Mradi kwa
wakati.
Aidha,
kwa miradi mingine inayosuasua inayohusu majengo ya shule na vituo vya
afya, Timu iliwataka wakandarasi husika kukamilisha kazi kwa wakati,
kuzingatia viwango na ubora.
Kuhusu
manufaa ya umeme, Mhandisi Luoga alieleza kuwa Mradi wa Rusumo
utakapokamilika utazalisha megawati 80 ambazo zitagawanywa kwa nchi tatu
zinazohusika ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi kwa kila moja kupata
megawati 27.
Alisema
kuwa kwa upande wa Tanzania, Mradi utasaidia kuongeza umeme katika
gridi ya Taifa pamoja na kuboresha hali ya upatikanaji nishati hiyo
katika Mkoa wa Kagera.
“Kama
alivyoelekeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, kuwa Mkoa
wa Kagera uingizwe katika gridi ya Taifa, hivyo kukamilika kwa Mradi wa
Rusumo kutawezesha hilo.”
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele,
akizungumza na Timu hiyo ofisini kwake kabla ya kuanza ziara, alipongeza
kazi nzuri inayoendelea kufanyika ambayo alisema imeleta manufaa
makubwa kwa wananchi wake.
“Miundombinu
ambayo imejengwa ni ya kipekee. Hatukuzoea kuona Shule za Msingi
zinakuwa na Jengo la Utawala lakini kupitia Mradi huu hilo limefanyika
na kwakweli inapendeza sana,” alifafanua.
Naye
Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya, Herman Hume alieleza
kuwa miradi hiyo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani Ngara
ilitengewa fedha kiasi cha dola milioni tano za Marekani ambazo ni sawa
na takribani shilingi bilioni 12 za Tanzania.
Wengine
wanaoshiriki katika ziara hiyo itakayoendelea kwa siku mbili nyingine
ni Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa
Rubagumya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Wajumbe wa
Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Rusumo.
Pia,
Timu imefuatana na Mhandisi Patrick Lwesya, Meneja Mradi wa Rusumo,
Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi
pamoja na Maafisa kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.
No comments:
Post a Comment