WANAWAKE
wa jamii ya wafugaji wa Kata ya Mundarara Wilayani Longido wamenufaika
kiuchumi baada ya kujihusisha na shughuli za uchenjuaji mchanga wa
madini ya Ruby.
Wakizungumza
wakati wakipatiwa elimu ya afya na usalama kwa wachekechaji iliyotolewa
na shirika la Haki Madini, wanawake hao walidai kuwa maisha yao
yamebadilika kiuchumi kupitia madini hayo ya Ruby wanayaopata baada ya
kuchekecha mchanga.
Mmoja
kati ya wachekechaji hao Martha Ngada alisema kupitia uchekechaji huo
amefanikisha kuwasomesha watoto wake saba akishirikiana na mumewe.
Ngada
alisema hivi sasa wameondokana na utegemezi kwa kubadili maisha yao
kiuchumi kupitia mchanga wa madini ya Ruby wanayochenjua mgodini.
"Pia nimefanikiwa kuwanunua mbuzi watano ambao ninaendelea kuwafuga na kujipatia maziwa ambayo nakunywa na kuyauza." alisema.
Mchekechaji
mwingine Leah Lazaro alisema shida ndogo ndogo ameondokana nazo hivi
sasa kupitia kazi yao ya kuchenjua mchanga wa madini ya Ruby.
Lazaro
alisema wanawake wengine wanapaswa kubadilika kwa kufanya kazi halali
ya kujipatia kipato kuliko kujihusisha na vitendo visivyo na maadili au
kuomba mitaani.
Ofisa
miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise alisema katika elimu
waliyotoa pia wametoa barakoa kwa wanawake hao ili waweze kujikinga na
vumbi.
Mbise
alisema wamewapa elimu wanawake hao wasifanye kazi ya kuchekecha
mchanga wakiwa na watoto wao kwani watawasababishia maradhi ya vifua.
Ofisa
ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Longido, Atuganile Chisunga
alisema wanawake wengi wa eneo la Mundarara wamejiunga na shughuli za
uchenjuaji mchanga baada ya kubaini kuna kipato.
Ofisa
jinsia na uchimbaji wa shirika la Haki Madini, Joyce Ndakaru alisema
hivi sasa jamii ya wafugaji wanawake wanaimudu kazi hiyo kutokana na
kutotumia nguvu kubwa.
"Kupitia
mradi wa afya na usalama unaotekelezwa kwenye vijiji vinne vya eneo
hili tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na wanawake katika
kujishughulisha," alisema.
No comments:
Post a Comment