Prisca
Joseph, Neema Yeremia kutoka kikundi cha Sauti ya Mwanamke chini ya
SPRF, wakiwa na familia ya binti aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia,
kijijini kwao mangaa, ikungi, Kulia ni Mratibu wa Field wa Shirika lisilo la kiserikali la JIOKOE na UMASKINI ‘SPRF’ (yaani Stars of Poverty Rescue Foundation), Bernard Maira.
Baba Mzazi wa muathirika wa tukio akiwa na huzuni.
Wana
kikundi cha Sauti ya Mwanamke chini ya SPRF, wakiwa na familia ya binti
aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia, kijijini kwao mangaa.
Na Godwin Myovela, Singida
“Nilizibwa
mdomo wangu huku nikiwa nimekandamizwa kwa nguvu shingoni, yule kijana
alikuwa ameshika panga na akaniambia endapo nitathubutu kupiga kelele
basi atakata shingo yangu, sikuwa na msaada wowote, hatimaye
alinibaka...nashindwa kusimulia uchungu na maumivu makali
niliyoyapata.”
Ni
maneno ya kutia simanzi kwa binti wa miaka 14, mwanafunzi wa darasa la
saba wa shule ya Msingi Mungaa (jina limehifadhiwa). Mnamo Januari
2019 akiwa anarudi nyumbani akitokea shuleni, mwendo wa takribani nusu
kilometa baada ya masomo yake, ghafla kati ya njia alikutana na kijana
mmoja anayeishi kijijini hapo.
Kijana
huyo ambaye naye (jina limehifadhiwa) akaanza kumshika-shika huku
akimvuta kwa nguvu na kumnyonga mikono yake kumpeleka pembeni ya
barabara mahali ambako hapakuwa na watu.
“Nilibaki
nikitetemeka na kujikuta nikiishiwa nguvu, sikuweza tena kupiga kelele
wala kulia kwasababu nilielekezewa panga, akanibaka! Na baada ya tukio
jamaa akatoweka. Ndipo mimi nikapata nafasi ya kujikongoja kuelekea
nyumbani huku miguu yangu yote ikiwa inachuruzika damu,” anaeleza Mhanga
wa tukio hilo.
Nikiwa
njiani huku nikilia kwa uchungu nilijiuliza nitaanzaje kuwaeleza
wazazi? Na vipi endapo nitapata ujauzito? Na je kuhusu hatma yangu ya
masomo itakuwaje? Kwakweli nilichanganyikiwa sana kupitia tukio lile la
kinyama; Lakini baada ya kupita miezi 4 kila kitu kilikuwa wazi”.
Kama
alivyotabiri binti, siku ile ya tukio ndivyo ilivyotokea… (siku ileile
aliyobakwa ndiyo aliyopata ujauzito). Binti akiwa shuleni alionekana
mjamzito na Mwalimu Mkuu aliandika barua kuwaita wazazi wake baada ya
kukamilisha hatua zote za kumchukua vipimo, ambavyo vilithibitishwa
pasipo shaka na madaktari kuwa binti alikuwa mjamzito.
Wazazi
waliitwa shuleni na kuelezwa mabadiliko walioyaona kwa binti huyo na
hatimaye walijulishwa kwamba binti yao ni mjamzito, na kwa mujibu wa
taratibu za shule hiyo hataweza tena kuendelea na masomo, hivyo warudi
naye nyumbani.
“Nilikaa
nyumbani hadi nilipojifungua. Nilipata wakati mgumu sana kipindi chote
cha ujauzito, na wakati wa kujifungua ililazimika nifanyiwe upasuaji
(operation) nikajifungua salama lakini kizazi changu kilionekana kina
matatizo hivyo kiliondolewa…hapa sina tena kizazi, kizazi changu
kimekwisha-ondolewa,” anasimulia binti huyo wa miaka 14 wakati huo huku
akitoa machozi.
Anasema
kinachomuumiza zaidi ni pale anapomuona mtuhumiwa aliyemfanyia ukatili
ule akiwa huru mtaani, na anaishi kwa furaha bila msaada wala habari
yoyote, hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa mpaka sasa licha ya tukio
kuripotiwa Polisi, na baadaye shauri hilo kupelekwa mahakama ya Utemini
mkoani Singida.
“Baada
ya kesi hii kuripotiwa kituo kidogo cha Polisi katika kijiji cha
Mungaa, na baadaye kupelekwa mahakama ya mwanzo Utemini mjini Singida;
kila shauri lilipokuwa likitajwa mahakamani tulijikuta tukihudhuria mimi
na wazazi wangu, yule kijana alikuwa hafiki…kwa kweli ilifika wakati na
sisi tukaishiwa nauli tukashindwa kuhudhuria hii kesi kila ilipokuwa
ikitajwa,” anasimulia huyo binti.
Binti
anasema mpaka kufikia tarehe 4 Februari mwaka huu, shauri hilo lilikuwa
halijatolewa hukumu yoyote, na yule kijana mpaka sasa yupo huru mtaani
huku binti yeye akiwa tayari amepoteza mwelekeo na ndoto zake zote za
maisha.
“Kwasasa
nafanya biashara ya kuuza kuni, hizi kuni huwa nazifuata umbali wa
kilometa tatu kutoka hapa nyumbani huku nikiwa na mtoto mgongoni,
nafanya hivi ili kutafuta kipato cha kunisaidia kuweza kumtunza
mwanangu; nauza kuni hizi shilingi elfu 2 kwa fungu moja,” anasema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la JIOKOE na UMASKINI ‘SPRF’
(yaani Stars of Poverty Rescue Foundation), katika kutekeleza mradi
wa AWARE ndio waliotoa taarifa ya tukio hili. Dkt . Suleiman Muttani, na
watendaji wenzake kupitia kikundi cha elimu na hamasa cha mradi wa
AWARE dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto,
maarufu ‘Sauti ya Mwanamke’ katika kijiji cha Mungaa ndio walioibua
sakata hilo.
Hata
hivyo, Dkt. Muttani anasema wanaendelea kuwasiliana na maofisa Ustawi
wa Jamii Wilaya ya Ikungi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
kisheria vinavyoshughulikia shauri hilo ndani ya mipaka yao, ili
kuhakikisha wanamsaidia mhanga aweze kupata haki yake stahiki.
“Mbali
na matukio mengine ya aina hii, mpaka sasa shirika letu limeibua
matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii takribani 56 yakiwemo
masuala ya ubakaji, vipigo kwa wanawake na watoto, mimba na ndoa za umri
mdogo na mengine ambayo chimbuko lake ni imani za kishirikina sanjari
na mila na desturi zilizopitwa na wakati kama ukeketaji ambao kwa sasa
unafanywa kwa siri kubwa kwa watoto wachanga usiku wa manane,” anasema
Dkt. Muttani.
No comments:
Post a Comment