MSAMAHA WA KODI YA VAT SEKTA YA KILIMO KUKUZA UZALISHAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 5, 2020

MSAMAHA WA KODI YA VAT SEKTA YA KILIMO KUKUZA UZALISHAJI

Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Antony Mtaka, ameiomba Wizara ya Fedha na Mipango kutoa msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mafuta ya kupikia yanayozalishwa hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo na tija kwa wenye viwanda.

Bw. Mtaka amsema kuwa hivi sasa Serikali imeondoa kodi kwenye mbegu za Mafuta jambo ambalo ni zuri lakini hatua hiyo ingekuwa na tija zaidi endapo kodi hiyo pia ingepunguzwa au kuondolewa kabisa kwenye Mafuta yanayozalishwa ili bei ya bidhaa hiyo iweze kupungua na kuchochea uzalishaji wa malighafi za kuzalisha Mafuta.

Hayo aliyasema alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Alisema kuwa Tanzania inaagiza Mafuta ya kupikia kwa kiasi kikubwa kutoka nje ya nchi hivyo msamaha wa VAT katika Mafuta hayo utasaidia kukuza uzalishaji, ushindani na kuokoa fedha zinazotumika kuagiza Mafuta hayo kutoka nje ya nchi.

“Kwenye pamba tunahamasisha kuongeza thamani, pamba izalishe nyuzi na mbegu izalishe Mafuta na tupate mashudu, sasa mbegu unaisamehe lakini Mafuta unatoza, bado tunatumia gharama kubwa sana kuingiza Mafuta toka nje”, alieleza Bw. Mataka.

Aidha kwa upande wa Taasisi ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT- AMIS), alisema kuwa kiwango cha Serikali kuhamasisha watu kununua hisa za taasisi hiyo iko chini na kuushauri uongozi wa Taasisi hiyo kutumia fursa ya wafanyakazi wastaafu hususan walimu ambao wanahitaji kuelimishwa ili washiriki katika ununuzi wa hisa za Serikali.

Alisema kuwa wastaafu wanapata changamoto kubwa hasa wanapoingia kwenye sekta binafsi na kujihusisha na ufugaji na biashara ya vyombo vya moto, baada ya mwaka mmoja wanafilisika ilihali kuna mahali ambapo angewekeza asilimia 60 ya mafao yake, angepata mshahara uleule kupitia hisa ambazo zingempa nafasi ya kukopa na kupata gawio kila mwezi.

Bw. Mtaka alisema kuwa katika ngazi ya Halmashauri, makundi ambayo Serikali inayagusa kama wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, taasisi za Wizara ya Fedha na Mipango zina nafasi kubwa ya kutoa ushauri wa namna ya kujitegemea, kwa kuwa kiasi cha asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kinachopelekwa katika makundi hayo tija yake bado ni ndogo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga, alisema kuwa Mifumo ya fedha iliyotengenezwa na watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, inaisaidia Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kusimamia mapato kwa kuwa  hali halisi ya ukusanyaji inaonekana hivyo kufanya wadau katika ngazi zote kufanya maamuzi sahihi ya matumizi yake na kuboresha vyanzo vya mapato.

Aidha Kodi 114 za sekta ya Kilimo na Mifugo zilizofutwa na Serikali zinachochea ongezeko la uzalishaji na kuwa na manufaa kwa wakulima katika kuongeza kipato na makusanyo kwa kuwa uzalishaji utaimarika.

Naye aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu. Bw. Jumanne Sajin, ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwaleta watumishi mahili kutoa elimu kuhusu masuala ya fedha, mifumo ya fedha, bajeti, Sera, Pensheni, mipango ya KItaifa, Ubia kati ya Umma na Sekta Binafsi pamoja na taasisi zake zilizo chini ya Wizara kwa kuwa elimu inayotolewa itachangia wananchi kuelewa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika Nyanja mbalimbali.

Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu yapo katika Siku ya tano na yanatarajia kumalizika Agosti 10 baada ya Waziri mwenye Dhamana ya Kilimo kuongeza siku mbili ili kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kushiriki na kujifunza.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Antony Mtaka (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta, alipowasili katika  Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Antony Mtaka (wa pili kulia) akiuliza maswali mbalimbli kuhusu miradi ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta, wa tatu kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Antony Mtaka (kulia), akieleza jambo kuhusu Mipango ya Kitaifa alipotembelea dawati la Mipango ya Kitaifa, wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta (kulia) akisikiliza ushauri kuhusu Vyuo kusaidia usimamizi wa maandiko ya miradi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Antony Mtaka (kushoto), alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka (wa nane kulia), Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta (wa tisa kulia), Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja (wa saba kuli), wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha, baada ya kutembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagin, akisikiliza maelezo ya Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Maendaenda (wa pili kushoto) alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagin, akifurahia jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja (kulia) baada ya kutolewa maelezo kuhusu takwimu za kilimo, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta (kulia) akipeana mkono na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagin, baada ya kukabidhiwa machapisho mbalimbali ya Chuo hicho, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagin, (katikati) akiwa katika picha ya Pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu. (Picha na Peter Haule, WFM)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad