Na Mwandishi Wetu,HESLB,DAR ES SALAAM
KATIKA kuhakikisha taifa letu
linajenga uchumi ulio imara na jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya
uwajibikaji na ubunifu, Serikali pamoja na mambo mengine imeendelea kuwekeza
katika elimu ya juu.
Serikali imeendelea kuhakikisha
Watanzania wote wenye sifa wanapata elimu ya juu kwa kupewa mikopo kupitia Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya Juu, iliyoanzishwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 9 ya
mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai, 2005.
Bodi ya Mikopo pamoja na
majukumu mengine, ina jukumu la kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wenye sifa
na wahitaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na mwombaji stahiki na
mhitaji anaweza kuomba mkopo /ruzuku ili kugharamia sehemu ya gharama au
gharama zote za masomo ya elimu ya juu.
Tangu kuingia madarakani kwa
Rais Dkt. John Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kuongeza bajeti ya
maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26
hadi asilimia 40 na hivyo kuweza
kupanua wigo na kuboresha upatikanaji wa huduma za mbalimbali za jamii ikiwemo elimu
ya Juu.
Katika
kipindi cha miaka mitano cha Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli Serikali
imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Tsh. bilioni 348.7 mwaka
2014/2015 hadi Tsh. bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020.
Kutokana
na msukumo na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali katika kuboresha elimu ya
juu nchini, Serikali imeiwezesha na kuijengea uwezo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu kutekeleza vyema majukumu yake ya kisheria na kuongeza uwazi na
ufanisi katika upangaji, utoaji na
ukusanyaji wa mikopo.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2020/2021, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema katika kipindi
cha mwaka wa fedha 2019/20, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu hadi kufikia machi 2020 imetoa
mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 449.99 kwa wanafunzi 132,119 sawa na
asilimia 99 ya fedha iliyoidhinishwa.
Prof. Ndalichako anasema katika ya hao, wanafunzi 49,799 ni wa mwaka wa
kwanza na 82,320 wanaoendelea na masomo hatua inayolenga kutoa fursa na kupanua
wigo kwa wanafunzi wenye sifa za uhitaji kujiunga na masomo katika vyuo na
taasisi za elimu ya juu nchini.
Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako anasema HESLB katika mwaka 2019/2020 pia imefanya
ukaguzi kwa waajiri 2,406 nchi nzima na kutambua wanufaika wapya 14,731 wenye
mikopo iliyoiva yenye thamani ya Shilingi Bilioni 100.7 ambapo kati yao
wanufaika 13,969 (94%) wameanza kulipa.
‘Aidha, hadi kufikia
Disemba, 2019 idadi ya wanufaika wanaorejesha mikopo ilikuwa imefikia 176,952
kati ya 184,166 waliotarajiwa sawa na asilimia 96 ya lengo’’ anasema Prof.
Ndalichako.
Kwa mujibu wa Waziri
Ndalichako anasema Bodi ya Mikopo imeendelea na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva
ambapo kiasi cha Tsh. Bilioni 144.3 kati ya Tsh. Bilioni 166.1 zilizolengwa
katika kipindi cha mwezi Juni 2019 hadi Machi 2020 sawa na asilimia 86.9
zimekusanywa, ambapo lengo la makusanyo kwa mwaka lilikuwa ni kiasi cha Tsh. Bilioni 221.5.
Prof. Ndalichako
anasema katika kusogeza huduma ya mikopo ya elimu ya juu karibu na wananchi
pamoja na pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva, HESLB
imefungua ofisi ya Kanda katika Mkoa wa Mtwara na kufikisha jumla ya ofisi sita
zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Mtwara, Mbeya na Zanzibar.
Akifafanua Zaidi
Prof. Ndalichako alisema Bodi ya Mikopo imeendelea kuboresha mifumo ya
uendeshaji ili kuongeza uwazi na ufanisi wa utoaji huduma katika upangaji,
utoaji na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva, ambapo kwa sasa mifumo hiyo
inamuwezesha mwanafunzi kupata taarifa za mkopo wake kupitia simu ya mkononi au
mtandaoni na kuondoa usumbufu wa wanafunzi kufuatilia taarifa hizo kwenye ofisi
za Bodi.
‘Bodi imebuni mfumo
unaoviwezesha vyuo kuambatisha nyaraka muhimu kama vile matokeo ya mitihani
kupitia mtandao badala ya kutuma nakala ngumu, vilevile uboreshaji wa mifumo
umehusisha uunganishaji wa mifumo ya TEHAMA ya Bodi ya Mikopo na ya Tume ya
Vyuo Vikuu ambapo taarifa za udahili za waombaji wa mikopo zinapatikana kwa
urahisi na kwa wakati’’ alisema Prof. Ndalichako.
Ni dhahiri kuwa wigo
wa utoaji elimu nchini unapanuka, hivyo ili kulinda ubora wa elimu ni wajibu wa
mamlaka zote zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa ubora wa elimu zitekeleze
majukumu yao ipasavyo kwa kutoa miongozo na kufanya kaguzi za mara kwa
mara.
(Mwandishi
ni Afisa Mawasiliano Mwandamizi HESLB, anapatikana kwa ingayonga@heslb.go.tz)
No comments:
Post a Comment