HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 27, 2020

WAZIRI BITEKO AZINDUA VIWANDA VIWILI VYA MFANO VYA UCHENJUAJI WA DHAHABU

WAZIRI wa Madini Doto BitAeko katikati akijiandaa kukata utepe hafla ya uzinduzi wa viwanda hivyo vya Mfano.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kilipojegwa kiwanda cha kuchenjua dhahabu bila kutumia kemikali ya zebaki cha Katente wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika tarehe 26 Aprili, 2020
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akiongea jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu vya Katente na Lwamgasa uliofanyika Katente mkoani Geita tarehe 26 Aprili 2020.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idrisa Kikula akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente wilayani Bukombe mkoani Geita tarehe 26 Aprili, 2020.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico Lucas Seleli akizungumza jambo mara baada ya uzinduzi na makabidhiano ya Viwanda viwili vya uchenjuaji wa Madini ya dhahabu kisichotumia kemikali ya zebaki vilivyoko Katente na Lwamgasa mkoani Geita.
Viongozi wa Serikali kuanzia kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akifuatiwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na mwisho ni Mshauri mwelekezi aliyesimamia ujenzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu Rogers Sezigwa wakiendelea na ukaguzi wa kiwanda hicho kabla ya kukikabidhi rasmi kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Mtaalamu wa kuendesha mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia teknolojia ya Kisasa Gabriel Masanyiwa akitoa maelezo ya hatua zinazopitiwa mpaka kupata dhahabu.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita mara baada ya hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente na Lwamgasa Mkoani Geita. Kiwanda hicho kimekabidhiwa kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ili kukisimamia na kukiendesha.

Waziri wa Madini, Doto Biteko amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kusimamia ipasavyo Viwanda vya Mfano vya Uchenjuaji wa madini ya dhahabu vya Katente-Bukombe na Lwamgasa-Geita alivyovizindua leo APRIL 26 na kuvikabidhi rasmi kwa shirika la Stamico..

Ujenzi wa viwanda hivyo visivyotumia kemikali hatari ya zebaki ulifanywa na kampuni ya Tan Discovery MineralConsaltancy Limited inayosimamiwa na Rogers Sezigwa iliyoanza ujenzi wa mradi mwezi Disemba, 2016 ikianziaLwamgasanakufuatianaKatentenaItungi- Chunya.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa viwanda hivyo vya Mfano,Waziri Biteko amesema, itakuwa aibu kubwa kwa Stamico endapo Viwanda hivyo vitafia mikononi mwao kwani Serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wa viwanda hivyo.

“Afe Kipa, afe beki ni lazima viwanda hivi vifanye kazi” Biteko alisisitiza.

Aidha,Waziri Biteko amewahakikishia wananchi na wachimbaji wadogo wa madini nchini kuwa, serikali ya Rais John Magufuli inawajali na itawahudumia kwa gharama nafuu hivyo wasisite kupeleka mawe kiwandani hapo ili waweze kuchenjuliwa dhahabu kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa na hivyo kuepuka kutumia zebaki na kuachana na utumiaji wa matimba kwenye mashapo.

Amesema matumizi ya matimba wakati wa uchimbaji yanasababisha uharibifu wa mazingira wakati zebaki huathiri afya za wachimbaji hivyo waitikie na kuvitumia viwanda hivyo kwa faida zao.

“Tumetengeneza viwanda hivi kuwavutia ninyi fanyebiashara” Biteko alisisitiza.

Pamoja na hayo, Waziri Biteko alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi hii pasipo kucheka na watu wasiotimiza wajibu wao kwenye viwanda hivyo.

Sambamba na hayo amewataka Bodi pamoja na Stamico kuhakikisha wananchi wanaozunguka viwanda hivyo wananufaika na uwepo wa viwanda katika maeneo yao kwa kupata ajira ndogo ndogo kwa kufanya hivyo kutainua uchumi wao.

Akizungumzia faida zitokanazo na uwepo wa viwanda hivyo vya mfano, Waziri Biteko alisema ni pamoja na utoaji wa mafunzo na maarifa kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo, kutolewa elimu ya mfumo wa kuthamini mashapo ya madini yaliyopo ilikufanya uchimbaji wenye tija, kuchenjua dhahabu pamoja na kukodishwa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji kwa gharama nafuu pamoja na kutolewa elimu juu ya uongezaji thamani madini na upatikanaji wa masoko.

Akizungumzia mchakato wa ujenzi wa viwanda hivi vya mfano, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal amesema, ujenzi huo nimatokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 iliyosisitiza zaidi juu ya uendelezaji wa sekta ya madini hususani wachimbaji wadogo.

Amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali ilianzisha mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) uliokuwa na awamu mbili, ya kwanza ni kuanzia 2009 hadi 2014 na awamu ya pili mwaka 2015 hadi 2018 ambapo awamuya pili ya mradi ndipo viwanda vitatu vya mfano vya uchenjuaji wa dhahabu vya Katente- Bukombe, Lwamgasa- Geita na Itumbi –Chunya vilipoanza kujengwa baada ya kufanyika kwa utafiti wa kijiolojia chini ya ushirikiano baina ya uongozi wa mradi, Stamico, Taasisi ya Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST) na wachimbaji wadogo.

Akizungumzia gharama ya ujenzi wa viwanda hivyo Ollal alisema mradi wa Katente umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na Lwamgasa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.3 wakati mradi wa Itumba Uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na hivyo kufanya miradi yote kutekelezwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 4.7.

Ollal ameongeza kuwa, uwepo wa tekinolojia hii kwa wachimbaji wadogo itakuwa na manufaa kama vile; kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali migodini kwa kutumia sementi katika kuimarisha kuta, kurahisisha utoaji wa mbale mgodini(Haulage system) kupunguza athari za kimazingira kwa kutokata miti hovyo na kurahisisha ufungaji wa migodi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara y aMadini, Prof. Simon Msanjila amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuisaidia jamii inayozunguka viwanda hivyo vya mfano kuondokana na changamoto ya maji kwa kuchimba kisima kiwandani hapo na kuiruhusu jamii kunufaika na huduma hiyo.

Aidha, Prof. Msanjila amewataka Stamico kutoa nafasi za ajira kwa wananchi kutokana na ukweli kwamba wao ndio walinzi wa viwanda hivyo. “Nitashangaa sana kuona wafanyakazi wakawaida wanatoka km 200 kutoka hapa wakati kijiji kimezungukwa na vijana mahiri na wachapa kazi” alisistiza Prof. Msanjila.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ametoa wito kwa watendaji na wasimamizi wa vituo hivyo kuwa wazalendo katika usimamizi wa Viwanda hivyo vya uchenjuaji wa dhahabu.

Sanjari na hilo, ameelezea mikakati ya mkoa wake kuelekea maonesho ya Tekinolojia ya uchimbaji wa madini kwa mwaka huu kuwa ni pamoja na mkoa wake kuandaa uwanja maalum kwa ajili ya maonesho hayo ambapo tayari ujenzi wa jengo la ofisi mbalimbali ikiwepo ya wataalamu wa Sekta ya madini umefanyika.

Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wataalamu na timu nzima ya Ujenzi wa viwanda hivi kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo ili kuachilia utaalamu wao kwa watanzania wengine wenye nia ya kujiendeleza kupitia sekta ya Madini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad