Zingatieni Maadili ya kazi katika utekelezaji wa majukumu yenu – CGP Kasike - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 16 October 2019

Zingatieni Maadili ya kazi katika utekelezaji wa majukumu yenu – CGP Kasike

Na ASP Lucas Mboje, Masasi
KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike amewaasa Maafisa na askari wote wa Jeshi hilo kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi na nidhamu Jeshini. 
Amesema hayo leo alipotembelea katika magereza ya Namajani, Masasi na Gereza Newala katika ziara yake ya kikazi Mkoani Mtwara yenye lengo la kujionea utendaji kazi wa Jeshi hilo katika vituo mbalimbali vya Jeshi hilo.

Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa wapo baadhi ya maafisa na askari ambao wanatatizo la kimaadili na hawataki kubadilika hali ambayo inaharibu taswira ya Jeshi hilo katika jamii.
 "Taswira ya Jeshi la Magereza inategemea zaidi utekelezaji mzuri wa majukumu yenu kwa kuzingatia maadili na nidhamu. Jukumu letu ni kusimamia wafungwa ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza adhabu zao kwa mujibu wa Sheria, " alisema Kamishna Jenerali Kasike.

Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amekemea tabia ya ulevi wa kupindukia kwa baadhi ya maafisa na askari kwani tabia hiyo inachangia sana katika kushuka kwa maadili ndani ya Jeshi hilo.
“Nitaendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu ikiwemo kuwafukuza kazi Maafisa na askari ambao hawataki kubadilika kwani vitendo vya ukiukaji maadili havikubaliki Jeshini,” Amesisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Varisanga Msuya amemhakikishia Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza kuwa atahakikisha kuwa Maafisa na askari katika Mkoa wake wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika uendeshaji wa Jeshi hilo. 

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike, kesho Oktoba 17, 2019 ataendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Mtwara ambapo anatarajia kutembelea Gereza Kiwanda Chumvi kabla ya kuhitimisha ziara yake Gereza Kuu Lilungu.
 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akizungumza na Maafisa na askari wa Gereza Namajani lililopo Wilayani Masasi, leo Oktoba 16, 2019 alipotembelea katika ziara yake ya  kikazi Mkoani Mtwara.
 Baadhi ya askari wa Gereza Namajani wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike.
  Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akizungumza na Maafisa na askari wa Gereza Masasi, leo Oktoba 16, 2019 alipotembelea katika ziara yake ya  kikazi.
 Mkuu wa Gereza Masasi, Mrakibu wa Magereza, Juma Mkumba akitoa taarifa fupi ya Gereza  mbele ya Kamishna Jenerali wa Magereza nchini(hayupo pichani) alipotembelea Gereza hilo.
 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili toka kushoto) akikagua Mifugo katika Gereza Namajani lililopo Wilayani Masasi, leo Oktoba 16, 2019 alipotembelea katika ziara yake ya  kikazi Mkoani Mtwara.
 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akiwasili Gereza Newala, leo Oktoba 16, 2019 alipotembelea gereza hilo.
 Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na askari wa Gereza Namajani alipotembelea leo Oktoba 16, 2019 katika ziara yake ya  kikazi. Kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Varisanga Msuya(Picha zote na Jeshi la Magereza).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad