HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 8 October 2019

JUMLA YA WAGONJWA 28,876 WENYE MATATIZO YA MOYO WATIBIWA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

Jumla ya wagonjwa 28,876 wenye matatizo ya moyo wametibiwa kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba mwaka huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo Dkt. Peter Kisenge wakati akieleza taarifa ya kazi zilizofanywa na Kurugenzi yake katika kikao cha menejimenti kilichofanyika jana katika Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi hiyo wanaume walikuwa 12,566 na wanawake 16,310 ambapo 6,590 sawa na asilimia 22.8 walikuwa wagonjwa wapya.

“Tumeona wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi za Ethiopia, Malawi, Zimbabwe, Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wagonjwa waliotibiwa na kurudi nyumbani walikuwa 27,882 na wagonjwa 994 walilazwa kati ya hao 500 ni wanawake na 494 ni wanaume idadi ya vifo vikiwa ni asilimia 6”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge aliendelea kusema kuwa watoto waliotibiwa katika Taasisi hiyo walikuwa 1,516 ambapo wa kike walikuwa 800 na wavulana 716 kati ya hao wagonjwa 374 walikuwa wapya.

Dkt. Kisenge alisema, “Wagonjwa wengi tuliowaona walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo,valvu, matundu, mishipa ya damu ya moyo na magonjwa ya moyo ya kuambukizwa yanayosababisha makovu katika valvu za moyo kutokana na kupata mafindofindo kwenye tezi za koo (Rheumatic Heart disease) ”,.

Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo pamoja na kuwekewa vifaa vinavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri walikuwa 352 kati ya hao watoto 87 sawa na asilimia 24.7 na hakukuwa na mgonjwa aliyepoteza maisha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji Dkt. Anjela Muhozya alisema wamefanya upasuaji kwa wagonjwa 153 kati ya hawa wagonjwa 122 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua, wagonjwa 23 walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya damu na nane walifanyiwa upasuaji wa mapafu.

“Tumefanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao valvu zao zilikuwa na shida, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo na kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft – CABG). Wagonjwa waliopoteza maisha ni watatu sawa na asilimia 2.5”, alisema Dkt. Anjela.

Dkt. Anjela alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika matibabu ya wagonjwa wa moyo ni wagonjwa wengi kufika katika Taasisi hiyo huku mioyo yao ikiwa imechoka. Na kuwaomba wagonjwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujuwa kama wanamatatizo ya moyo au la na kama watakuwa nayo waweze kupata matibabu kwa wakati.

Naye Cecilia Nthala kutoka nchini Malawi ambaye mtoto wake anatibiwa katika Taasisi hiyo alishukuru kwa huduma ya matibabu ya moyo aliyoipata .

“Nilipata taarifa ya Taasisi hii kupitia tovuti na mitandao ya kijamii, kwa kuwa mtoto wangu ana matatizo ya moyo nikawa nafuatilia kwa ukaribu huduma mbalimbali wanazozitoa baada ya kuridhika nazo nikaamua kumleta mwanangu ili naye apate huduma ya matibabu”, alisema Cecilia.

“Kwa kipekee ninawashukuru wauguzi na madaktari kwani muda wote wako karibu na mimi najiona kama vile niko nchini kwetu Malawi. Ninawaomba muendelee kutoa huduma kama hii mliyoitoa kwangu kwa wagonjwa wengine mnaowatibu”, alishukuru Cecilia.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad