HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 19, 2019

TEGESHA YAWAUMIZA KICHWA WATHAMINI FIDIA NYAMONGO

Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Zoezi la uthamini kulipa fidia kwa wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu North Mara kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Taka limekumbwa na changamoto kufuatia baadhi ya wananchi kujenga nyumba ama kuongeza sehemu za nyumba zao maarufu kama ‘Tegesha’ ili kujipatia faida kupitia thamani ya fidia.

Wathamni katika zoezi hilo walibaini tofauti kubwa katika uthamini walioufanya awali na pale walipoenda kwa mara ya pili kwa ajili ya uhakiki ambapo ilibainika baadhi ya vyumba katika nyumba zilizofanyiwa uthamini kuwa wazi baada ya waliokuwa wakiishi kuondoka baada ya kuthaminiwa.

Imeelezwa kuwa lengo wananchi wanaofanya ujanja wa ‘Tegesha’ ni kujipatia posho ya makazi ambayo kwa kawaida hutolewa kama fidia kwa wamiliki kulingana na idadi ya vyumba kwenye nyumba ya mmiliki.

Kwa mujibu wa Wathamini wa zoezi hilo, mbali na wamiliki walioathirika na zoezi hilo kulipwa gharama nyingine kama vile nyumba na mazao pia hulipwa posho ya makazi kwa kipindi cha miezi 36 lengo kumuwezesha mpangaji kupata mahali pa kuishi kabla ya kuanza zoezi la kuondolewa.

Mwandishi wa Gazeti hili alishuhudi moja ya nyumba iliyopo kitongoji cha Kigonga A katika kijiji cha Matongo ikiwa na vyumba ishirini na moja wakati nyumba hiyo ilistahili kuwa na vyumba vitatu na baadhi ya vyumba havina hata madirisha.

Mthamni Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha ambaye alitembelea baadhi ya nyumba hizo kukagua maendeleo ya kazi ya uthamini katika eneo hilo aliweka wazi kuwa Ofisi yake inafanya kazi kwa kufuata sheria ya Uthamini na hatua kali zitachukuliwa kwa mtu atakayeonekana kufanya udanganyifu kwa kwa lengo la kujipatia kipato.

Kwa mujibu wa Mugasha, zoezi la uthamini katika eneo la Nyamongo linalohusisha vitongoji vitatu katika kijiji cha Matongo limekuwa likifanyika kwa uwazi na kushirikisha pande zote wakati wa kuorodhesha mali na kufafanua kuwa hata mwananchi asiyeridhika na uthamini katika eneo lake hupewa fomu maalum ya kujaza lengo likiwa kutoa haki.

‘’Tumeona watu walihamisha magodoro, vitanda na mizigo mingine lengo ni kupata posho ya makazi ili kujipatia faida na cha kushangaza baadhi ya wapangaji hawajui hata choo cha nyumba wanayoishi kilipo, ofisi yangu haitavumilia vitendo hivyo kila mtu atalipwa anachostahili’’ alisema Mugasha.

Mthamini kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Lazaro Magumba alieleza kuwa wakati zoezi la uthamini kumekuwa na changamoto hasa wakati wa kukagua mali za wananchi kutokana na baadhi yao kuwa na dhana ya kujipatia utajiri kupitia mradi huo ambapo hufanya maendelezo ya kuegesha maarufu kama ‘tegesha’ ili kulipwa fedha nyingi.

‘’ Wananchi wanajenga nyumba zilizopangana na hakuna hata nafasi na wakati wa uthamni usiku kucha watu wanahamisha vyombo, magodoro na wengine hata wanyama ili ionekane ni makazi halali’’ alisema Lazaro.

Alisema wanachokifanya wao ni kukagua kwa awamu kwa lengo la kujiridhisha kama kweli walionekana wakati wa uthamini kama ni wakazi halali ama walienda kutegesha.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matongo wilayani Tarime mkoa wa Mara ambao hawakupenda majina yao yawekwe wazi kutokana na sababu za kiusalama walikiri kuwepo mchezo huo wa Tegesha lakini walidai hufanywa na watu wasio wakazi wa muda mrefu katika kijiji hicho bali walienda kwa lengo la kujipatia faida kupitia zoezi hilo.

Kwa mujibu wa wakazi hao, baadhi ya wananchi kutoka nje ya kijiji hicho walinunua nyumba ama maeneo kwa wenyeji na kuongeza vyumba na kuwakodisha watu kuishi ili kuvizia zoezi la uthamini wa fidia wapate faida.

Kwa muda mrefu wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale wanaoishi vitongoji vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja kutoka Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya zao jambo lililomlazimu Rais John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika eneo hilo kuagiza kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
  Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akiwa katika chumba kilichojengwa maarufu kama Tegesha katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi.
 Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akionesha moja ya chumba kilichojengwa maarufu kama Tegesha katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (Wa pili kushoto) akiongozana na timu ya uthamini katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad