HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 19, 2019

NI MUHIMU KUWEKEZA KWENYE TEHAMA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ili kuleta maendeleo endelevu ya viwanda, kuongeza biashara na kutengeneza ajira, nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kuwekeza katika uunganishaji na uwianishaji wa viwango mbalimbali vya TEHAMA.

Amesema hatua hiyo itasaidia kutatua changamoto za maendeleo ya miundombinu na muingiliano wa mawasiliano nje ya mipaka ya nchi na kikanda. “Changamoto hizo zinajumuisha maunganisho ya njia kuu za mawasiliano kati ya nchi jirani, kuyafanya mawasiliano ya kikanda yabaki ndani ya kanda, maunganisho ya kuvuka mipaka ya nchi, upangaji wa bei pamoja na uwianishaji wa viwango.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 19, 2019) wakati akifungua Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa SADC wa sekta ya TEHAMA, uchukuzi na hali ya hewa pamoja na kongamano maalumu la Mawaziri, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema kwa kipindi hiki, nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha kuwa utekelezaji unalenga katika teknolojia zinazochipukia kwenye utoaji wa huduma za posta sambamba na kuanzisha huduma na bidhaa mpya ambazo zitakidhi mahitaji ya sasa ya wateja na kuhamasisha biashara mtandao.

“Katika kufanikisha hili, ni muhimu kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Posta wa SADC wa mwaka 2017-2020 ambao uliridhiwa mwezi Septemba, 2017.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ili kufikia mtangamano wa kikanda kuhusua miundombinu ya usafiri na usafirishaji, mkutano huo unapaswa kuzungumza namna gani nchi wanachama zinaweza kuwianisha sera, viwango, mifumo ya sheria katika maeneo ya barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini, pamoja na hali ya hewa.

Waziri Mkuu amesema kuna haja ya kuboresha miundombinu muhimu ya usafirishaji, utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa vitu na huduma pamoja na kuwezesha kutoa mizigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ndani ya kanda. “Hivyo, nawaomba katika mkutano wenu mjadili maeneo haya na kuja na mapendekezo ya suluhisho ili kutatua vikwazo mbalimbali.”

“Tanzania imeweza kuboresha miundombinu ya bandari pamoja na mifumo ya uendeshaji ili kusaidia nchi za SADC ambazo hazipakani na bahari nazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Malawi pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Jamhuri za Uganda, Rwanda na Burundi.”

Waziri Mkuu amesema kuwa nchi wanachama wa SADC zinapaswa kuboresha mifumo ya reli kwa kuzingatia Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kikanda wa mwaka 2015-2063 pamoja na Mpango Kamambe wa Maendeleo ya Miundombinu wa Kikanda wa mwaka 2019-2023.

Amesema kati ya miradi mikubwa inayotekelezwa hapa Tanzania, ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendo kasi inayojengwa katika ukanda wa kati pamoja na ukarabati wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ambayo inaunganisha nchi wanachama wa SADC. “Hivyo, katika ukarabati uliofanyika wa TAZARA, umeongeza uwezo wa reli hiyo kusafirisha mizigo kutoka tani 88,000 mwaka 2014/2015 hadi tani 220,000 mwaka 2017/2018.”

Mkutano huo unahudhuriwa na Mawaziri wa Sekta ya TEHAMA, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa kutoka nchi za Angola (4), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (2), Msumbiji (1) Zambia (3), Afrika Kusini (2), Lethoto (1), Zimbabwe (2) na Tanzania inawakilishwa na Mawaziri watano na Naibu Waziri Mmoja, akiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, wakati akiwasili kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Gabriel Mukungu, wakati akiangalia mfumo wa unaorahisisha mawasiliano kwa vyombo vya usafiri (Traffic Information System - TIMS), kabla ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa, uliyofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 19.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mfumo wa unaorahisisha mawasiliano kwa vyombo vya usafiri(Traffic Information System - TIMS), kabla ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa, uliyofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 19.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Injinia James Kilaba, nje ya ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, kabla ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia gari maalum la mtambo wa usimamizi wa masafa, nje ya ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, kabla ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. Kulia ni Mhandisi Mwandamizi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Victor Kweka.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihutubia kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Mwakilishi wa Katibu Mkuu SADC, Mapalao Makuena, akizungumza kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mwakilishi wa Katibu Mkuu SADC, Mapalao Makuena (katikati), , nje ya ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, baada ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Paramagamba Kabudi, nje ya ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, baada ya kufungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi za SADC wa masuala ya Tehama, Uchukuzi, Habari na Hali ya Hewa. Septemba 19.2019. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad