HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 23, 2019

DAWASA YAWAVALIA NJUGA WAHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJI KAWE

MAMLAKA ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) leo Septemba 23 imekagua miundombinu ya maji katika Mikoa ya kihuduma ya mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe  na katika ukaguzi wao wameshuhudia wananchi wakitumia maji kwa njia udanganyifu na kusababisha hasara kwa wateja halali waliounganishwa na wanaolipa bili.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miundombinu ya maji katika mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe Meneja Mapato wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Edger Zawayo amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo ni vyema wanaohujumu miundombinu hiyo wakaacha mara moja kabla ya hatua kali za kisheria dhidi yao hazijachukuliwa.

Zawayo amesema kuwa mmoja wa watuhumiwa wa kuhujumu miundombinu ya maji amekamatwa na atafikishwa mahakani na sheria itafuatwa ili liwe fundisho kwa wengine.

Amesema kuwa wananchi wazitumie ofisi za mamlaka hiyo kwa kupata huduma ya maji na sio kuhujumu huduma hiyo kwa wateja ambao wameshalipia huduma zao.

"Tutaendelea kuwashughurikia wale wote ambao wanahujumu miundo mbinu ya maji na hatutawafumbia macho maana wanasababisha hasara kubwa kwenye mamlaka hiyo" Alisema Zawayo

Amesema kuwa kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake kwa kutoa taarifa kwenye ofisi za Serikali za mitaa na ofisi za DAWASA zilizokaribu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Amesema kuwa adhabu kwa wahujumu wa miundombinu hiyo ya maji ipo palepale, yaani faini  kuanzia shilingi milioni tano hadi hamsini, na amewashauri wananchi kuwa waaminifu ili kutokutwa na kadhia hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Muzimuni Hassan Ngonyani  amewaasa wananchi wa mtaa huo juu wa wizi wa maji wanaoufanya  badala yake wafuate taratibu maalumu na kupata huduma hiyo ya maji kwa uhalali.

Amesema kuwa wananchi wote wanaohitaji huduma ya maji watumie ofisi zilizopo kila mahali na ni vyema wakafuata taratibu na kulipa bili na sio kuhujumu maji kwa wateja halali na kuwasababishia hasara.
  Mtaalamu wa Mambo ya Mita kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Da es Salaam (DAWASA) Mohammed Mwakimila(kushoto) akionesha bomba la maji lililokuwa limeunganishwa kwenye bomba la mteja kinyemela na kuelekezwa kwenye Duka la Dawa lililopo katika mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe leo wakati ukaguzi wa miundombinu ya maji ya Mamlaka hiyo. Katikati ni Mwenyekiti wa mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe, Hassan Ngonyani na  Mtaalamu wa Mambo ya Mita kutoka Idara ya Biashara ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Da es Salaam DAWASA Martin Kulembe(kulia) wakishuhudia tukio hilo.
 Mtaalamu wa Mambo ya Mita kutoka Idara ya Biashara ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Da es Salaam DAWASA Martin Kulembe(katikati) akionesha wizi uliokuwa unafanywa kwa mteja anayetuhumiwa kujiunganishia maji pamoja na Mwenyekiti wa mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe, Hassan Ngonyani(kulia) wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya maji katika mtaa huo.
 Mwenyekiti wa mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe, Hassan Ngonyani akizungumza na wafanyakazi wa DAWASA pamoja na baadhi ya wateja wa Mamlaka hiyo mara baada ya kujionea wizi uliokuwa unafanyika kwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka hiyo wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya maji katika mtaa wa Muzimuni kata ya Kaweleo jijini Dar es Salaam.
 Sehemu ya maungio ya maji ya wizi yalipokuwa yakichukuliwa kutoka kwenye bomba la mmoja wa wateja wa DAWASA likitoka maji mara baada ya kulikata bomba hilo wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya maji katika mtaa wa Muzimuni kata ya Kaweleo jijini Dar es Salaam.
 Moja ya mita ya maji ikiwa ndani ya nyumba kinyume na utaratibu wa mita kukaa nje ya nyumba ili kuondoa udanganyifu na wizi wa maji.
Mita ya maji ya DAWASA ikiwa imeunganishwa mambomba mengi na bila kutumia utaratibu uliowekwa na mamlaka hiyo haya yote yalibainika mara baada ya maofisa wa DAWASA kufanya ukaguzi katika mtaa wa Muzimuni kata ya Kawe.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad