HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 20, 2019

UBALOZI WA MAREKANI WAITWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani hapa Nchini Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias alipomwita Wizarani kutoa ufafanuzi kuhusu angalizo la kiusalama lilitolewa na ubalozi huo kupitia tovuti ya Ubalozi wa Marekani hapa Nchini June 20, 2019.

Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ulitoa taarifa katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert”. Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi unaodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulimwita wizarani Kaimu Balozi wa Marekani ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao. Ubalozi wa Marekani ulimtuma Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias kuonana na uongozi wa Wizara. 

Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias ameutambua na kukiri kuwa ujumbe huo umetumwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini. Katika ufafanuzi wake amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.

 Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo  nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
14 Juni 2019

1 comment:

Post Bottom Ad